Miss Tanzania namba mbili 2006, mwanamitindo na mcheza filamu, Jokate Mwegello, akiwa katika picha ya pamoja na watoto wanaolelewa katika Kituo cha Yatima cha Extrem cha Tandale kwa Bi Mwamvua Jumanne, alipotembelea kuwapa zawadi ya Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya. Zawadi alizotoa ni mchele, unga wa sembe, sabuni na ndala zenye nembo za Kidoti.
MISS Tanzania namba mbili 2006, mbunifu mavazi na muigizaji wa
filamu za kibongo, Jokate Mwegelo ‘Kidoti’, jana ilitoa msaada wa vitu
mbalimbali katika Kituo cha Kulea Yatima cha Extreme kilichopo Tandare
kwa Bi Mtumwa, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mrembo huyo ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya Kidoti
inayojihusisha na masuala ya urembo, alitoa msaada huo kama zawadi yake
ya Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya kwa watoto hao kama sehemu ya
kuwafariji ili nao kujiona wako sawa na wengineo wanaioshi nawazazi wao.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Jokate alisema kuwa
ameguswa na kituo hicho ambacho huwa hakikumbukwi na wahisani kutokana
na mazingira ya eneo hilo.
“Nimefika hapa kutoa msaada kama sehemu ya kuonyesha ninavyoguswa na
jamii ya watoto kama hawa, lakini pia nikiwa na lengo la kuwafariji ili
nao kujiona ni sehemu ya jamii ya Watanzania,” alisema.
Kidoti alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watu wenye uwezo, kampuni
na taasisi mbalimbali kuona umuhimu wa kusaidia makundi hayo maalumu
katika jamii kwani nao wana haki ya kuishi na kufurahia maisha kama
wengine.
Misaada aliyokabidhi kwa ushirikiano na kampuni ya Rainbow Shell, ni
mchele, unga wa sembe, sabuni, jozi za viatu vyenye nembo za Kidoti.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, mlezi wa watoto hao, Mwamvua
Jumanne, alitoa pongezi kwa Kidoti na kuwasihi wengine kuiga mfano wa
mrembo huyo kusaidia makundi maalum.
Akielezea changamoto zilizopo katika kituo hicho, Mwamvua alisema ni
kukosa uwezo wa kifedha kuwalipia ada watoto wanaosoma elimu ya msingi
na sekondari, gharama za matibabu pamoja na kukosa watu wa kuwatembelea
ili kuwafariji.
(Picha na Jumanne Juma).
|
Post a Comment