SERIKALI YAMJIBU LISSU MADAI YA BOMBADIER KUSHIKILIWA KISA MADENI
Kufuatia madai mazito yaliyotolewa na Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki na mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwamba ndege ya serikali aina ya Bombadier iliyotakiwa kutua nchini mwezi Juni, imezuiliwa na watu wanaoidai serikali, Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, imetoa taarifa ya kupinga vikali kauli ya Lissu na wenzake na kutoa ufafanuzi.
Katika taarifa iliyotolewa leo, Agosti 19, 2017 katika Ukumbi wa Idara ya Habari, Maelezo, msemaji mkuu wa serikali amewahakikishia Watanzania kuwa ndege hiyo ipo na itakuja nchini, na kwamba taratibu za kidiplomasia na za kisheria zinaendelea ili kuhakikisha kuwa ndege hiyo inakuja nchini na kuanza kutoa huduma.
Aidha, katika taarifa hiyo, msemajai mkuu wa serikali, amewataka wananchi kuwa makini na wanasiasa wanaotafuta umaarufu, kwani zipo taarifa zinazoonesha kwamba wanasheria walioizuia ndege hiyo, walishawishiwa na wanasheria kutoka nchini, wasioitakia mema serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
“Wanasheria hao waliokwenda kufungua madai kwamba serikali yetu inadaiwa na kwamba ndege hiyo ishikiliwe, hawana uhalali wowote wa kufanya hivyo na ni matapeli tu ambao wamesukumwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wasioitakia mema nchi yetu,” ilikaririwa sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo iliendelea kueleza kwamba, wapo wanasiasa nchini ambao wanakingia kifua mambo ambayo yanarudisha nyuma maendeleo ya nchi, ikiwemo kuwashawishi wafadhili wasilete misaada tena Tanzania, kubeza jitihada za kunusuru madini na maliasili za nchi na wanaobeza juhudi za Rais Magufuli katika kuhakikisha kuwa maisha ya Watanzania, hasa wa hali ya chini, yanaboreshwa.
Post a Comment