CHADEMA YALALAMIKIA MAHAKIMU KUWANYIMA DHAMANA WANACHAMA WAKE
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelalamika dhidi ya baadhi ya mahakimu wanaokataa kupewa dhamana viongozi na wanachama wake wanaokabiliwa na kesi katika mahakama mbalimbali nchini.
Malalamiko hayo yamo katika taarifa iliyotolewa leo na chama hicho kwenda kwa Kaimu Jaji Kuu Mahakama ya Rufani, Prof. Ibrahim Juma, iliyosema hali hiyo inalenga kuwakomoa viongozi na wanachama wa Chadema ambao wamefunguliwa kesi za uchochezi na mikusanyiko haramu. “Kesi za aina hiyo zimekuwa nyingi kufuatia amri ya Rais John Magufuli kukataza vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara.
Na sasa hata baadhi ya mikutano ya ndani inakatazwa na viongozi wa kisiasa kama wakuu wa wilaya na wa mikoa pamoja na jeshi la polisi,” imesema sehemu taarifa hiyo ambayo imetolewa pia kwa vyombo vya habari.
Ikisisitiza, taarifa hiyo imesema katika kadhia hiyo baadhi ya mahakimu wanawanyima dhamana au wanawawekea masharti magumu ya dhamana au wanachelewa kuwapa dhamana bila sababu za msingi katika kesi mbalimbali ambazo wamefunguliwa nchini.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Makamu Mwenyekiti wa Taifa (Bara) wa Chadema, Prof. Abdallah J. Saffari, imetaja baadhi ya kesi zinazowakabili viongozi na wanachama wa Chadema.
Post a Comment