Ashinda Ubunge kimaajabu

                                                               Kijana John Paul Mwirigi aliyeshinda Ubunge.

Kijana John Paul Mwirigi mwenye umri wa miaka 23 na mwanafunzi wa chuo kikuu cha Mt. Kenya, ameibuka mshindi wa Ubunge wa jimbo la Igembe nchini Kenya bila ya kubandika hata kipeperushi kimoja cha kujipigia kampeni.
John ambaye alikuwa mgombea binafsi ni mwanafunzi wa shahada ya ualimu, ameshinda kwa kura 18,897 akifuatiwa na mgombea wa chama cha Jubilee Rufus Miriti ambaye amepata na kura 15, 411.
John Mwirigi ambaye anatarajiwa kuwa mbunge mwenye umri mdogo zaidi amesema alikuwa anafanya kampeni kwa kutembea nyumba hadi nyumba na baadaye kuungwa mkono na madereva boda boda ambao walimsaidia kufanya hivyo, huku akiwataka watu kumtambua kwenye karatasi za kupigia kura akiwa amevalia sweta lake la rangi ya kijivu na mstari wa blue nyeusi kifuani, ili wasikosee.
“Nataka niwashukuru watu wa jimbo la Igembe Kusini kwa kunichagua, nitawatumikia kwa uwezo wangu wote nikishirikiana na wenzangu kwa sababu lengo langu ni kuwawakilisha wananchi wa kawaida ambao matatizo yao hayatazamwi na wabunge wakishaingia ofisini”, alisema John Mwirigi.
John ambaye anajiita ‘Hustler wa kawaida’, amedai kipindi chote hicho kabla ya uchaguzi alikuwa hana kazi maalum ili alikuwa anategemea vibarua vya kawaida hivyo amemshukuru Mungu pamoja na wananchi waliompigia kura na kuwaahidi hatoweza kuwaangusha.
Hata hivyo, Nafasi ya mbunge mwenye umri mdogo zaidi nchini Kenya ilikuwa inashikiliwa na Boniface Kinoti Gatobu ambaye alikuwa na umri wa miaka 26 alipoingia bungeni kwenye bunge la 11, na sasa John anatarajiwa kuchukua nafasi hiyo mara baada ya kuapishwa.

No comments

Powered by Blogger.