NSAJIGWA KOCHA MPYA YANGA
NAHODHA na mchezaji wa zamani wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, rasmi ni kocha msaidizi wa timu hiyo.
Nsajigwa aliyekuwa anaifundisha timu ya vijana ya U20 anakuwa kocha wa timu hiyo akichukua nafasi ya Juma Mwambusi aliyekuwa anakinoa kikosi hicho.
Yanga inaachana na Mwambusi baada ya mkataba wa kuendelea kuifundisha timu hiyo kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara.
Championi Jumatano, lilimshuhudia Nsajigwa jana akiwa kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Nsajigwa alionekana akitoa baadhi ya maelekezo kwa wachezaji wa timu hiyo akisaidiana na kocha wa viungo wa timu hiyo, Mzambia, Noel Mwandila.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili limezipata, kabla ya mazoezi hayo kuanza Nsajigwa alitambulishwa kwa wachezaji wa timu hiyo.
“Nsajigwa rasmi ni kocha msaidizi wa Yanga atakayekuwa anasaidiana na Lwandamina, Mwandila na Mwambusi hatakuwepo na timu hiyo tena,” alisema mtoa taarifa huyo.
Gazeti hili mara baada ya mazoezi hayo kumalizika, lilimtafuta Nsajigwa kuthibitisha hilo, akasema: “Mimi sina taarifa rasmi juu ya hilo suala la kuwa kocha msaidizi, tusubirie kwanza kama ikiwa hivyo basi nitatoa taarifa rasmi.”
Post a Comment