Kibiti hali si shwari: Mmoja auawa kikatili

                              Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji, Onesmo Lyanga 

 Kukiwa bado kuna hali ya sintofahamu kuhusu mauaji yanayoendelea mkoa wa Pwani huku Serikali kupitia jeshi lake la Polisi ikijitahidi kuwabaini watu hao wanaotekeleza mauaji hayo bado kitendawili cha kuwabaini watu hao hakijapata jibu.
Kitendawili hicho hakijateguliwa kwa kuwa usiku wa kuamkia jana, mkazi mmoja wa Kitongoji cha Nyambwanda katika Kijiji cha Hanga wilayani Kibiti, Hamis Ndikanye (54) ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake.
Tukio hilo linafanya idadi ya watu ambao wameuawa mpaka sasa kwa kupigwa risasi mkoani Pwani kufikia 38 wakiwemo Askari polisi 13 kitu ambacho Watanzania wanabaki na hofu kubwa na maisha yao hususani katika mkoa huo.
Katika tukio hilo la usiku wa kuamkia jana, Hamis Saidi ambaye ni ndugu wa marehemu amesema watu hao wanaodhaniwa kuwa watano wakiwa na bunduki walifika nyumbani kwa Ndikanye saa sita usiku na kufanya mauaji hayo.
Saidi amesema watu hao baada ya kufika nyumbani kwa ndugu yake, waligonga mlango wa nyumba yake wakimtaka afungue lakini aligoma ndipo wahalifu hao waliamua kuvunja mlango huo kwa kitu kizito na kisha kuingia ndani na kumkuta Ndikanye akiwa amelala na mkewe.
Saidi amesema kabla ya kufanya mauaji hayo ya ndugu yake wahalifu hao walimfunga mkewe kwa kitambaa usoni na mikononi, kisha kumpiga marehemu risasi mbili zilizosababisha kifo chake.
Mganga wa Kituo cha Afya Kibiti, Dk Sadock Bandiko amethibitisha kifo hicho kwa kusema katika uchunguzi alioufanya kwenye mwili wa marehemu, alikuta majeraha wawili yaliyotokana na kupigwa risasi mbili, moja kichwani na nyingine mgongoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji, Onesmo Lyanga amesema tayari polisi wamekwenda Nyambwanda kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo.
Chanzo:Mwananchi
By Godfrey Mgallah

No comments

Powered by Blogger.