Katibu Mkuu CHADEMA aongezewa makosa
Katibu Mkuu wa (CHADEMA) Dkt. Vincent Mashinji
Katibu Mkuu wa (CHADEMA) Dkt. Vincent Mashinji ambaye leo amefika katika ofisi za Mkuu wa Polisi Ruvuma kuhojiwa juu ya tuhuma za kufanya mkutano bila kuwa na kibali huku kiongozi huyo wa chama akiongezewa kosa jingine la kutoa lugha ya kuudhi.
Dkt Mashinji ameongezewa kosa hilo leo kuwa alitumia lugha ya kuudhi pale aliposema "Watanzania hawapaswi kumwachia shamba ngedere kwa sababu madhara ya kumwachia shamba ngedere yanajulikana"
Katika tuhuma hizo mpya Mashinji anapaswa kutoa maelezo alikuwa akimaanisha nini na anapaswa kumtaja huyo ngedere ni nani, lakini katika taarifa iliyotolewa na Afisa habari wa (CHADEMA) zinasema viongozi wote 9 watafikishwa mahakamani leo mjini Songea.
"Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Katibu Mkuu Dkt. Mashinji pamoja na hao viongozi nane watafikishwa mahakamani leo mjini Songea. Chama kimeshaagiza timu ya wanasheria inayoongozwa na Wakili Mbogoro, kuhakikisha viongozi hao wanapata msaada wa kisheria ili haki itendeke kuanzia katika hatua hiyo ya mahojiano yanayoendelea na iwapo watawapelekwa mahakamani" alisema Tumaini Makene
Katibu Mkuu wa CHADEMA pamoja na viongozi wengine nane wa chama hicho walikamatwa na polisi mwishoni mwa wiki Mbamba - Bay wilayani Nyasa mkoa Ruvuma na kukaa rumande kwa masaa 48 kutokana na maagizo kutoka juu na waliachiwa siku ya Jumatatu jana na kupaswa kuwasili siku ya Jumanne leo kwa Mkuu wa Polisi Ruvuma kwa mahojiano zaidi.
credit: eatv.tv
credit: eatv.tv
Post a Comment