KAPOMBE ASHUSHWA AIRPORT DAR, AKIMBIZWA MUHIMBILI

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kuondoka Juni 19, mwaka huu kwenda Rwanda kwa ajili ya mchezo wa marudio dhidi ya Rwanda ambapo beki Shomari Kapombe
atalazimika kubaki Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Daktari wa Taifa Stars, Richard Yomba amesema kuwa Kapombe alikuwa akisumbuliwa na nyonga, lakini alijitonesha katika mchezo uliopita wa Taifa Stars dhidi ya Rwanda uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Amesema watakapotua Dar wakitokea Mwanza, Kapombe atabaki ili apelekwe kwa watalaam katika Hospitali ya Muhimbili kwa vipimo zaidi wakati wenzake wakielekea Rwanda.
Amesisitiza kuwa ataachwa hapo kufanyiwa vipimo kujua ukubwa wa tatizo lakini tangu aumie ameshindwa kufanya mazoezi.
Stars itaondoka Mwanza kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania majira ya saa nne asubuhi na kuwasili Dar es Salaam majira ya saa sita mchana kabla ya kuunganisha ndege ya Rwanda majira ya saa nane alasiri kwenda Kigali, Rwanda.
Inakwenda Kigali kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Rwanda maarufu kama Amavubi kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN 2018). Fainali za CHAN mwakani zitafanyika nchini Kenya.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Mshindi wa jumla katika michezo miwili, atakuwa amesonga mbele hivyo kukutana na Uganda mwezi ujao.

No comments

Powered by Blogger.