Makonda Kujenga Vituo 20 Vya Kisasa Vya Polisi Dar

 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na wananchi Kituo cha Polisi cha Tandika, Dar.
                                    ..Maongezi yakiendelea katika Kituo cha Polisi cha Tandika.
            Makonda akizungumza na mmoja wa mahabusu alipotembelea vituo vya polisi.




                                                        Kituo cha Polisi Kigogo, Dar.

Muonekano wa Kituo cha Polisi Traffic Mwenge, Dar.

Tangu kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi na taarifa za changamoto zifuatazo kuhusu hali ya huduma za kipolisi mkoani kwake;-
1. Wananchi kutokupatiwa huduma kwa saa 24 kutokana na vituo hivyo kufungwa usiku.
2. Mazingira mabovu na yasiyoridhisha ya vituo vya polisi.
3. Polisi kutofika kwenye matukio kwa wakati pindi wapigiwapo simu na wananchi.
4. Polisi kushindwa kutoa huduma kutokana na upungufu wa askari polisi.
5. Majambazi kuvamia vituo vya polisi wakiwa na lengo la kuchukua silaha.

Changamoto hizi za msingi na ambazo zinahatarisha uhakika wa usalama wa raia wa Dar es Salaam na mali zao ndizo hasa zimemsukuma Makonda jana kufanya ziara maalum ya kutembelea baadhi ya vituo vya polisi ili kujionea hali halisi, ambapo baada ya ziara hiyo pamoja na mengineyo amebaini kuwa kuna ulazima wa kujenga vituo vikubwa zaidi  vya kisasa, vinavyoweza kuhudumia wananchi wengi zaidi na kwa wakati, vilivyounganishwa na huduma za kisasa za mawasiliano na utunzaji kumbukumbu na vinavyoweza kutumiwa na idadi kubwa zaidi ya polisi akiamini kuwa ujenzi huu una maana kubwa katika kuzalisha majawabu ya sehemu kubwa ya changamoto zilizotajwa.
Kwa sababu hiyo, Makonda ametangaza kuanza mchakato wa ujenzi wa vituo 20 vya polisi vitakavyogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 10 ikimaanisha ya kwamba kwa kila kituo zitatumika shilingi milioni 500 pesa ambazo mkuu wa mkoa anapanga kufanya mazungumzo maalum na wadau wa maendeleo wa mkoa wake ili wamchangie sawa kabisa na namna alivyopambana kupata pesa za kutekeleza miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa mkoani kwake, ikiwemo ujenzi wa wodi tatu za kisasa, Makao Makuu ya BAKWATA na majengo ya emergencies hospitalini, miradi ambayo inagharimu zaidi ya shilingi bilioni 25 za Kitanzania, fedha ambazo hazitoki kwenye mfuko wa serikali bali kwa wadau wanaounga mkono utendaji wa Makonda unaoyapa kipaumbele maslahi ya wananchi wa Dar kwa ukubwa wake.
Kwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umegawanyika katika wilaya  tano, kwa kila wilaya vitajengwa vituo 4 na kila kituo kitakuwa na ofisi za kisasa, vyumba vitatu vya mahabusu (kimoja cha wanaume, kingine cha wanawake na cha tatu ni kwa ajili ya wale wenye mahitaji maalum), chumba cha mahojiano, vyumba vya silaha, idara ya usalama barabarani (traffic), mapokezi, dawati la jinsia na ofisi za teknolojia ya mawasiliano (ICT sections), kwa ukubwa wake kituo kimoja kitatumiwa na idadi ya askari wasiopungua 100.
Makonda amezitaka Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam wapeleke mchanganuo wa maeneo ambayo vituo hivyo vitajengwa ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma za ulinzi na usalama za uhakika na kwa wakati wote kwa lengo la kudumisha amani na utulivu katika mkoa wetu wa Dar es Salaam.

No comments

Powered by Blogger.