Umeya Kinondoni: Chadema Wafungua Kesi Mahakamani Wakidai Uchaguzi Haukuwa Halali
Viongozi wa Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) wamekimbilia mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi
wa umeya na naibu meya wa Manispaa ya Kinondoni katika Jiji la Dar es
Salaam uliompa ushindi Diwani wa Msasani, Benjamin Sitta wa CCM kuwa
Meya.
Ukawa kupitia kwa Wakili wao, John
Mallya wamewasilisha kesi hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, Dar es Salaam kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 23
mwaka huu, kwa kuwa ulikuwa batili na ulikiuka taratibu za kisheria.
Mallya alisema kesi hiyo ambayo
walalamikaji ni aliyekuwa Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Jumanne Mbunju na
aliyekuwa mgombea wa umeya, Diwani wa Kata ya Kinondoni, Mustafa Muro,
imepokelewa lakini haijafunguliwa.
Mbali na Sitta, walalamikiwa wengine
katika kesi hiyo ni Naibu Meya, Manyama Mangaru, Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli na Ofisa Tawala
wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza baada ya kesi hiyo
kupokelewa, Wakili Mallya alisema wamefungua kesi hiyo kupinga kile
wanachoita uchaguzi ambao CCM walikaa wenyewe na kupigiana kura.
Alisema: “Katika kesi hiyo
tunaiomba Mahakama itengue uamuzi uliomchagua meya huyo, iamuru manispaa
iitishe uchaguzi wa umeya mara moja pia imuamuru Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Manispaa na wasimamizi wa uchaguzi wafuate taratibu za
kisheria.”
Katibu wa Chadema mkoa wa Dar es
Salaam, Henry Kileo alisema wamefika mahakamani kutafuta haki kwa sababu
wanaamini wamenyang’anywa haki yao.
Alisema kilichosababisha uchaguzi wa
Ubungo kuahirishwa ni kukiukwa kwa taratibu hivyo Mkurugenzi na Ofisa
Tawala wa Ubungo walipoona taratibu zimekiukwa Kinondoni, waliamua
kuahirisha uchaguzi.
“Kilichofanyika siku ile ilikuwa ni
kuchagua Mwenyekiti wa CCM, lakini siyo uchaguzi wa kumchagua meya wa
Kinondoni kwa sababu hata kisheria, uchaguzi unatakiwa kuwa robo tatu ya
wajumbe ambao walitakiwa kuwa 23, lakini walikuwa 18, ndiyo maana hata
matokeo yalikuwa kura 18,” alisema.
Alidai madiwani wao walinyimwa fursa
ya kuingia manispaa na kuwasilisha malalamiko yao hivyo hawamtambui Meya
wa Kinondoni na kwa sasa hakuna Meya wa Manispaa hiyo.
Post a Comment