Manji na Wenzake Wawasilisha Pingamizi Dhidi ya IGP Sirro, AG Masaju na Mkuu wa Upelelezi DSM

Mwenyekiti wa Makampuni ya Quality Group ya jijini Dar es Salaam, ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji na wenzake wawili wamefungua kwa hati ya dharura maombi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar wakiomba waachiliwe kwa sababu wamekamatwa isivyo halali.
 Katika maombi hayo yaliyowasilishwa leo Julai 4, 2017 na kupangiwa mbele ya Jaji Lugano Mwandambo, walalamikaji wengine ni Deogratius Kisinda na Thobias Fwere ambapo wamefungua maombi hayo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, IGP Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi Kanda ya DSM.

 Hati ya kiapo ambayo imewasilishwa na Wakili Gudson Ndusyepo, Manji na wenzake wanaiomba Mahakama Kuu iwaachie kutokana na kukamatwa isivyo halali huku wakiiomba Mahakama hiyo kutoa amri ya kuwataka walalamikiwa wawafikishe Mahakamani ili washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

 Katika hati hiyo, Wakili Ndusyepo amebainisha kwamba Manji na wenzake walikamatwa nyakati tofauti ambapo mlalamikaji Kisinda alikamatwa June 30, 2017 majira ya saa 10 jioni huku Manji na Fwere walimatwa July 1, 2017 saa 5 asubuhi katika Jengo la Quality Center Barabara ya Pugu, DSM.

 Manji na wenzake walikamatwa kwa tuhuma za kukutwa na sare za Jeshi katika ghala la Quality Motors Group ambapo kupitia hati hiyo ya kiapo, Wakili Ndusyepo amebainisha kuwa kukamatwa kwa walalamikaji sio halali kwa sababu kosa linalodaiwa dhidi yao linahusiana na masuala ya Kampuni ya Quality Motors ambayo inaongozwa na Wakurugenzi wake na Manji.

 Mara baada ya kukamatwa kwa walalamikaji hao waliombewa dhamana lakini ilikataliwa kwa sababu zisizojulikana:

 “Kama Wakili wa waombaji nimefuatilia suala la dhamana hadi sasa saa 48 zimeshapita tangu walipokamatwa, lakini hawajafikishwa Mahakamani. Jambo hilo ni kinyume na sheria.” – Wakili Ndusyebo.

No comments

Powered by Blogger.