SOMA TEGETE ALIVYOWATISHA WEKUNDU WA MSIMBAZI
MSHAMBULIAJI wa
Mwadui FC Jerryson Tegete amekiri mchezo wa leo dhidi ya Simba utakuwa
mgumu kwavile wapinzani wao wapo kwenye kiwango bora huku wao wakihitaji
ushindi kwa hali yoyote baada ya kukusanya pointi nane kwenye michezo
yao minne ya mwisho iliyoshuka dimbani.
Tegete alisema matokeo
hayo yamewaongezea morali wachezaji katika mchezo huo utaofanyika kwenye
uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga ambapo kwa pamoja wameamua
kuisimamisha Simba ambao katika michezo yao 11waliyocheza hawajapoteza
mchezo hata mmoja na kutoka sare miwili pekee.
Akizungumza na BOIPLUS
Tegete alisema kuwa timu yao imeanza kurudi kwenye mstari baada ya
kuyumba katika mechi kadhaa zilizopita na sasa kuelekea kumalizika kwa
mzunguko wa kwanza wamejipanga kuhakikisha kumchapa kila atakayepita
mbele yao wakianza na Simba.
“Lolote linaweza kutokea
tulikuwa katika kipindi kigumu lakini sasa timu imeanza kukaa sawa kama
umeona mechi zetu nne za mwisho tumetoka sare mbili na tumeshinda
mbili, mechi ya tano ni dhidi ya Simba nayo tumejipanga kufanya vizuri,”
alisema Tegete.
Tegete ambaye alikuwa
akiifunga Simba mara kwa mara wakati akiichezea Yanga alisema tangu
aondoke Yanga amecheza mechi moja tu dhidi ya Wekundu hao msimu
uliopita na hakufanikiwa kuwafunga ila kama atapewa nafasi ya kucheza
kesho itakuwa ngumu kwa safu ya ulinzi ya Simba kumzuia asicheke na
nyavu.
Mwadui imefunga mabao 9
tu katika michezo 11 hali inayoashiria kuwa hawana safu imara ya
ushambuliaji huku Simba wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu pekee
kitu kinachompa ugumu Tegete kupita kwenye safu hiyo ngumu iliyo chini
ya Method Mwanjale na Juuko Murshid.
Post a Comment