MWIGULU NCHEMBA ATOA SIRI ILIYOSABABISHA PLUIJM KUBWAGA MANYANGA YANGA
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ameweka hadharani
kilichomkasirisha Kocha Hans van der Pluijm hadi akaamua kuachia ngazi
kuinoa Yanga.
Mwigulu ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga, ndiye aliyekutana na Pluijm
na kumshawishi kubadili uamuzi wake wa kubwaga manyanga kuinoa Yanga.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, kiongozi huyo na kada wa CCM,
amesema Pluijm alikasirishwa na Yanga kumleta kocha George Lwandamina
wakati yeye akiwa bado kazini.
“Alikarishwa na hilo, aliona analetwa kocha mwingine. Aliponieleza, nikazungumza naye na kumshawishi kubadili uamuzi wake.
“Lakini nilipozungumza na uongozi wa Yanga, nao wakaonekana hawakuwa na tatizo hata kidogo na wanamheshimu sana kocha.
“Kikubwa nimeona kama Yanga wanataka kufanya mabadiliko, wanaweza
kufanya hivyo hapo baadaye, mfano wakati wa mapumziko na si sasa
katikati ya ligi.
“Tena utaona kocha waliyenaye anafanya vizuri, amefanya vizuri kwa kuchukua makombe yote msimu uliopita,” alisema Mwigulu.
“Mwenyekiti (Yusuf Manji), hata yeye alisema haikuwa sahihi kocha ambaye
ameweka heshima Yanga kuondoka kwa staili hiyo. Hivyo mwisho
tumeafikiana na yeye ataendelea na kazi.”
Mara baada ya kutua kwa Lwandamina, Pluijm aliamua kuachana na Yanga kwa kuandika barua ya kubwaga manyanga.
Post a Comment