Mtihani wa Kidato cha Nne kuanza leo.......NECTA Yatoa Onyo
Watahiniwa
408,442 wamesajiliwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kufanya
Mtihani wa Kidato cha Nne unaotarajia kuanza leo hadi Novemba 18, mwaka
huu.
Akizungumzia
maandalizi ya mtihani huo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde
alisema kati ya watahiniwa waliosajiliwa wa shule ni 355,995 na wa
kujitegemea ni 52,447. Mwaka 2015, waliosajiliwa kufanya mtihani ni
448,382, hivyo kuwapo na upungufu wa watahiniwa 39,940.
Dk
Msonde alisema kati ya watahiniwa wa shule 355,447 waliosajiliwa,
wavulana ni 173,423 ambao ni asilimia 48.72 na wasichana ni 182,572 sawa
na asilimia 51.28. Watahiniwa 59 ni wasioona na wenye uoni hafifu ni
283.
Alisema
kati ya watahiniwa wa kujitegemea 52,447 waliosajiliwa, wanaume ni
25,529 sawa na asilimia 48.68 na wanawake ni 26,918 sawa na asilimia
51.32.
Pia
watahiniwa wa kujitegemea wasioona wako saba, wanawake watatu na
wanaume ni wanne. Mwaka jana watahiniwa wa kujitegemea walikuwa ni
54,317.
Kuhusu
watahiniwa waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Maarifa (QT), Dk Msonde
alisema baraza limesajili 20,634 ambao wanaume ni 7,819 sawa na asilimia
37.89 na wanawake ni 12,815 sawa na asilimia 62.11. Mwaka jana, idadi
ya watahiniwa wa QT walikuwa 19,547.
“Maandalizi
yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na
usambazaji wa mtihani, vitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu
zinazohusu mtihani huo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani,” alieleza Dk Msonde.
Aidha,
baraza limewaasa wanafunzi, walimu kutojihusisha na vitendo vya
udanganyifu wa mtihani kwani watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa
hatua kali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufutiwa matokeo yote.
Katika
matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa wiki iliyopita, wanafunzi 238
kutoka shule sita walifutiwa matokeo yao yote kutokana na udanganyifu wa
mtihani.
Dk
Msonde alizitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri,
kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya Taifa
zinazingatiwa ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya
vituo yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha
udanganyifu. Pia Dk Msonde alitoa mwito kwa wasimamizi wote kufanya kazi
yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.
“Wasimamizi
wanaaswa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani baraza litachukua
hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji
wa Mitihani ya Taifa,” alieleza.
Post a Comment