Mambo Muhimu Waliyoyajadili Rais Magufuli na Rais wa Congo DRC Joseph Kabila wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari Ikulu
Katika
Mazungumzo hayo Rais John Pombe Magufuli amemuhakikishia Rais Joseph
Kabila Kabange kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua kadhaa za
kuimarisha huduma katika bandari ya Dar es Salaam na kupunguza vizuizi
vya barabarani hadi kubaki vitatu ili nchi ya Kongo na nchi nyingine za
kusini na magharibi mwa Tanzania ziitumie bandari hiyo bila vikwazo.
Dkt.
Magufuli amesema Tanzania imejiwekea malengo ya kuhakikisha uchumi wake
unakua kwa asilimia 7.2 na kwamba kutokana na hali hiyo anawakaribisha
wafanyabiashara wa Kongo kuja kuwekeza nchini Tanzania na
wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kuwekeza nchini Kongo.
“Mhe.
Rais Joseph Kabila Kabange takwimu zinaonesha nchi zetu zinafanya
biashara kubwa kwani katika mwaka 2009 tulifanya biashara iliyofikia
Shilingi Bilioni 23.1 na imekuwa ikikua mwaka hadi mwaka na hivi sasa
tunafanya biashara yenye thamani ya shilingi Bilioni 393.6 kwa mwaka
“Mimi
ningependa kuona sisi ndugu na majirani tunafanya biashara zaidi,
wafanyabiashara wa Kongo waje Tanzania kuwekeza na Serikali yangu
itawaunga mkono” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais
Magufuli amezungumzia mikakati ya kuimarisha mawasiliano ya barabara na
ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge)
ambapo Tanzania imetenga Shilingi Trilioni 1 kwa ajili ya kuanza ujenzi
huo na kwamba hatua hiyo itarahisisha zaidi usafirishaji wa mizigo ya
kwenda na kutoka Kongo kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akitambulisha viongozi kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016
Kuhusu
mradi wa ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi
bandari ya Tanga nchini Tanzania, Rais Magufuli amesema ni matarajio
kuwa Kongo ambayo pia imegundua mafuta katika ziwa Albert itatumia bomba
hilo kama ambavyo Tanzania pia inatarajia kulitumia kufuatia tafiti
kuonesha uwepo wa mafuta katika maeneo ya ziwa Eyasi na Ziwa Tanganyika.
Kwa
Upande wake Rais Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Mhe. Jospeh Kabila
Kabange amemshukuru Rais Magufuli kwa mwaliko huu wa ziara ya kiserikali
na amemhakikishia kuwa Kongo itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano
wake na Tanzania kwa kuwa nchi hizi ni majirani na ndugu tangu enzi ya
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mhe. Kabila
amesema Kongo inatambua umuhimu wa kushirikiana na Tanzania katika
biashara na uwekezaji na kwamba amefurahishwa na hatua ambazo Serikali
ya Tanzania imezichukua kuboresha huduma katika bandari ya Dar es Salaam
ambayo ni tegemeo kwa usafirishaji wa mizigo ya Kongo Mashariki na
sehemu nyingine za nchi hiyo.
Ameahidi kuwa pamoja na kuwahasisha
wafanyabishara wa Kongo kuitumia bandari ya Dar es Salaam, Serikali yake
itachukua hatua za kurekebisha kasoro zinazolalamikiwa na
wafanyabiashara dhidi ya maafisa wa forodha wa Kongo waliopo hapa
nchini.
Rais Kabila amezungumzia mradi wa ujenzi wa bomba la
mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini
Tanzania akisema nchi yake pia imeamua kutumia bomba hilo kusafirisha
mafuta yake iliyoyagundua katika ziwa Albert upande wa Kongo na pia
juhudi zinazoendelea kupata mafuta katika ziwa Tanganyika na amesisitiza
kuwa ili kufanikisha hilo ushirikiano ni muhimu.
Kuhusu hali ya
usalama nchini Kongo, Rais Kabila amesema kwa asilimia 97 nchi hiyo ina
usalama na kwamba ni maeneo machache tu ya mashariki mwa Kongo ndiko
kuna vikundi vinavyoendesha vurugu.
“Mhe. Rais
Magufuli hivi karibuni tutaanza mazungumzo ya kutafuta amani ya kudumu
nchini Kongo, na lengo letu ni kuhakikisha nchi inakuwa na amani kabla,
wakati na baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Desemba ama baada
ya mwezi Desemba” amesema Rais Kabila.
Mhe. Rais
Kabila amekubali kuupokea ujumbe wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za
Tanzania, Angola na Msumbiji ambao Mwenyekiti wa asasi ya Siasa, Ulinzi
na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC – Organ
Trioka) Rais John Pombe Magufuli ataituma hivi karibuni kwa ajili
kufuatilia hali ilivyo nchini Kongo.
Baada ya mazungumzo rasmi na
kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, Rais Kabila
anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la jengo la Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari (TPA) lililopo kando ya Bandari ya Dar es Salaam na jioni
atashiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais John
Pombe Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Oktoba, 2016
Post a Comment