Hizi Team Kiba, Diamond ni Sumu
Diamond Platinums
Ali Kiba
Wiki iliyopita, wasanii Nasibu Abdul
’Diamond’ na Ali Saleh ‘Ali Kiba’ walikuwa ni kati ya wale waliopata
nafasi ya ushiriki wa Tuzo za MTV Mama ambazo zimefanyika nchini Afrika
Kusini na wote walipata nafasi ya kutumbuiza.
Na Saleh Ally
KAMA una simu inayoweza kufungua
mitandao ya kijamii, basi ukizubaa utakuwa na bahati ya kushuhudia
madudu tu na simu hiyo haitakuwa na faida kwako hata kidogo.
Mitandaoni kuna mambo mengi sana
yanaendelea na hayana maana hata kidogo ingawa wanayoyaendeleza huamini
wana uwezo mkubwa wa kuzungumza mambo na wanachosema ni sahihi hasa.
Kwenye Facebook, Instagram na Whatsapp ndiko jalala la kila asiye na
uwezo kufikiri au kutafakari na kulichambua jambo. Ili mradi kuna uhuru
wa kutoa maoni, basi kila mmoja ‘anatapika’ anachoona ni sawa. Hata vile
vilivyojaa ujinga, viko mitandaoni na huko vina thamani kubwa kwa kuwa
ndani ya mitandao hakuna kipimo cha madudu.Ali Kiba
Nimejifunza mengi na ajabu zaidi,
wachangiaji wa mambo mengi wasiojua mambo, hujirahisishia njia ya
uchangiaji kwa kuporomosha matusi.
Kutukana tu, ni sehemu ya kuonyesha
uwezo mdogo wa upambanuzi wa hoja pia inathibitisha mchangiaji ubongo
wake una njaa ya ufikiri kwa kiasi gani, lakini hauna uwezo wa kushiba
kabla ya kuendelea na kazi yake.
Diamond alitumbuiza na wacheza shoo
wake, Kiba akatumbuiza akiwa na Sauti Soul wa Kenya ambao
wamemshirikisha katika wimbo wao wa ‘Unconditional Love’.
Nianze kwa kuwapongeza Diamond na Kiba,
kwamba walifanya kazi nzuri kabisa. Mapungufu yalikuwepo kwa kila mmoja
wao, mfano Diamond sauti kuonekana ni kama ni mtu anayepumua kwa nguvu
lakini Kiba pia hakuwa na muda wa kutosha baada ya kuimba sehemu ya
ubeti wake na kiitikio ambacho kilipunguzwa. Haikuwa rahisi kuweza kuona
ubora wake vizuri lakini hakika, vijana hawa wa Kitanzania wanastahili
pongezi.
Shoo ya Diamond, ilikuwa bora kuliko
nyingine zote usiku huo ukumbini jijini Johannesburg, Afrika Kusini
lakini mitandaoni badala ya mjadala bora wa nani alifanya nini, kipi
kilipungua na wapi kiongezwe, matusi ndiyo yametawala.
Mimi niliweka video za vipande vya shoo
zao kwenye ukurasa wangu wa Instagram, lengo likiwa ni kuongeza
kuwasambaza na kuwatangaza vijana hao wa Kitanzania ambao wanaendelea
kuleta heshima na wanawapa changamoto wale ambao hawajafikia huko.
Diamond na Kiba si wasanii wa kwanza
kuleta heshima nchini lakini hadi wamefikia hapo lazima kabla walifikiri
kuwa kama fulani, mfano Lady Jay Dee au AY na wengine ambao walikuwa
wakifanya vema kimataifa.
Ajabu kabisa ni kwamba, walio mitandaoni
wanajulikana kama Team Kiba na Team Diamond. Hawa ni watu ambao wako
kwa ajili ya kusifia upande mmoja na kuupaka matope upande mwingine.
Team Kiba hakuna wanaloona ni zuri la
Diamond, Team Diamond kazi yao ni kuponda tu upande wa Kiba. Kila
unachofanya kama mwanadamu kinakuwa na faida zake, hasara zake pia.
Ukipima, utaona Team Diamond na Team
Kiba wanafanya kazi ya kupoteza muda, mambo ya kijinga pia ni watu
wasiotafakari kwa kuwa wamejivika kaniki na wanajaribu kuisafisha kwa
‘jiki’ ambalo si jambo sahihi.
Kaniki inakuwa jinsi ilivyo, kila
unapoifua ni lazima ukumbuke rangi yake, maana huwezi kuibadili kwa
kuifua. Si rahisi kuwaongezea au kuwapunguzia Diamond na Kiba kwa maneno
makali au matusi mitandaoni.
Kama Kiba na Diamond watakuwa wanazipa
nguvu hizo timu, basi hata wao watakuwa hawajui wanalolifanya na
hawafuatilii historia ya muziki kwamba wapambe kama hao Team Kiba na
Team Diamond, huko nyuma walikuwa ni sehemu ya kufa kwa makundi mfano
TMK Wanaume na East Coast TEAM.
Mashabiki badala ya kuburudika, wanaishi
na chuki, wanaamini kwenye kutukanana na kukataa kila kizuri cha
wanayemuona ni mpinzani. Hakuna wanaofanikiwa kwa kukataa mazuri ya
waliojitahidi.
Anayefanya vizuri, jifunze kwake. Pia
matusi hayajawahi kuingia kwenye historia yoyote ya mafanikio, badala
yake wanaofanya hivyo huonekana ni wendawazimu.
Vizuri kuepuka kugeuza mitandao kuwa
maficho ya wajinga na wanaoweza kusema lolote. Badala yake, kama kweli
nyie ni timu kwa ajili ya kuwasaidia wasanii hao ambao wote ni
Watanzania, basi muwe na mijadala bora yenye lengo ya kujenga, si kila
anayetukana ndiyo anaonekana hakuna kama yeye.
Kumbukeni hata hawa Diamond na Kiba,
siku moja watakwisha na wengine watapaa kwenye nafasi zao, hili halina
mjadala, hivyo mnaweza kuwasaidia kuendelea kubaki juu kwa muda mrefu
kwa mawazo bora, kukubali kazi ya mwingine na kukosoa kwa mlengo wa
uadui na chuki tu!
Vipi unaweza kuwa shabiki wa burudani,
halafu ukatumia muda wote kusambaza chuki wakati lengo namba moja la
burudani ni kuburudisha!
Post a Comment