Rais Magufuli afunga Maadhimisho ya Miaka 52 ya JWTZ ashuhudia Zoezi la Amphibious Landing Bagamoyo

  Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe
30 Septemba, 2016 amefunga maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ) kwa kushuhudia zoezi la medani liitwalo ''Amphibious Landing'' lililofanyika katika Kijiji cha Baatini
Wilaya ya Bagamoyo. Mkoani Pwani.


Zoezi hilo lililochukua
muda wa wiki mbili, limeshirikisha kamandi zote tano za JWTZ  ambazo ni Nyika, Majini, Anga, Kamandi ya
Makao Makuu na  Jeshi la Kujenga taifa limefanyika
katika ufukwe wa bahari ya Hindi na limetekelezwa kwa mfano wa mapambano ya
kivita yaliyohusisha kutua nchi kavu kutoka majini na kukomboa eneo
lililotekwa.
 
Akizungumza baada
ya kukamilika kwa zoezi hilo Rais na Amiri jeshi Mkuu Dkt.John Pombe Magufuli
amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange pamoja na
Makamanda na Wapiganaji wote wa JWTZ walioshiriki katika zoezi hilo ambalo
limefanywa kwa umakini, uhakika na weledi wa hali ya juu.
 
''Kwa kweli
nimefurahi na nimeamini tuna wapiganaji wa kutosha katika maeneo yote, hii
mikakati na mipango iliyotumika inaonesha tuna jeshi imara na linaloaminika''
amesema Dkt. Magufuli.  
 
Rais na Amiri
Jeshi Mkuu amewahakikishia Makamanda na Wapiganaji wote wa JWTZ kuwa Serikali
yake itahakikisha inaendeleza na kuongeza zaidi juhudi zilizofanywa na Marais
waliopita kwa kuimarisha na kuwa na jeshi la kisasa linalotumia vifaa na
teknoljia ya kisasa na pia itahakikisha maslai ya askari yanaboreshwa.
 
Aidha, Dkt.
Magufuli ametaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuimarishwa zaidi na kujielekeza
katika uzalishaji mali ikiwemo uwekezaji katika viwanda.
 
Maadhimisho hayo
yamehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali
Mohamed Shein ambaye pamoja na kuipongeza  JWTZ amesema miaka 52 tangu kuanzishwa kwa
Jeshi hilo Watanzania wanashuhudia jeshi lao likiwa imara na makini zaidi kwa
ajili ya kulinda nchi.
Nae Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange amemshukuru Rais na Amiri Jeshi
Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake na nia yake ya kuliimarisha
Jeshi na kuboresha maslai ya Makamanda na Wapiganaji na ameongeza kuwa
anajivunia kuwa kiongozi  wa Jeshi hilo.
 
Maadhimisho hayo
yamehudhuriwa na Viongozi wengine wakiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na
Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar Abdulhamid Yahaya Mzee.
 
Rais na Amiri
Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, amemuagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
Jenerali Davis Mwamunyange kuwapa ajira za JWTZ askari mgambo wote walioshiriki
zoezi la Amphibious Landing.


Gerson
Msigwa


Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU


Dar es
Salaam.


30
Septemba, 2016

 Amiri  Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Magufuli akipiga ngoma za bendi ya jeshi ya Mwenge Jazz wana Paselepa wakati  wa kufunga Zoezi la medani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016
 Amiri  Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na meza kuu wakipiga saluti wakati wa wimbo wa Taifa wakati wa kufunga Zoezi la medani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016
  Ndege vita zikipita angani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016
 Vifaru vinavyopita baharini na nchi kavu vikiwa katika zoezi la "Ambhibious Landing"  katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016
Amiri  Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na meza kuu wakipiga makofi wakati wa Zoezi la medani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016. PICHA NA IKULU.

No comments

Powered by Blogger.