Tundu Lissu Aibwaga Serikali Mahakamani
Serikali imeendelea
kupigwa mweleka katika kesi ya uchochezi dhidi ya mshitakiwa Tundu Lissu
baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupa pingamizi la Wakili wa
Serikali wakitaka wakili Peter Kibatala kujitoa kumtetea mwanasiasa
huyo.
Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema
alipandishwa kizimbani Agosti 5, na kusomewa mashtaka matatu, mawili
kati yake yakiwa ni ya uchochezi na moja la kuidharau mahakama.
Pigo la
kwanza la upande wa mashtaka ni pale Lissu alipopangua hoja na
kufanikiwa kupata dhamana, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani kwa
mara ya kwanza.
Jana ilikuwa ushindi mwingine kwa upande wa utetezi,
baada ya Mahakama kutupa pingamizi la upande wa mashtaka lililotaka
Kibatala ajitoe katika jopo la mawakili wanaomtetea Lissu.
Upande wa
mashtaka ulioongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi,
uliweka pingamizi hilo kwa maelezo Kibatala ni shahidi wao kwa kuwa
alikuwapo siku na mahali wakati Lissu akitoa maneno yanayodaiwa ya
uchochezi.
Wakili Kibatala ambaye ni kiongozi wa jopo la mawakili
wanaomtetea Lissu, alipinga hoja za Serikali za kutaka ajitoe katika
kesi hiyo, mvutano ambao ulisababisha kesi hiyo kuahirishwa mara mbili.
Wakili Kibatala alipinga kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachomzuia
wakili kumtetea mteja wake kwa sababu tu ya kushuhudia akitoa maelezo
yake Polisi.
Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo la Serikali, Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo, hakukubaliana na hoja
za upande wa Jamhuri (mashtaka) na hivyo akalitupa pingamizi hilo.
Hakimu Mkeha alikubaliana na hoja za wakili Kibatala kuwa hakuna kifungu
chochote cha sheria kinachomzuia kumtetea Lissu.
Alisisitiza kuwa
Kibatala ataendelea kuwa wakili wa Lissu katika kesi hiyo na kwamba
kama upande wa mashtaka ukimhitaji awe shahidi wao utalazimika kumuomba.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 19.
Post a Comment