WANAWAKE WALIOPONA FISTULA CCBRT WAAMUA KUJIAJIRI


 Bi. Kwenge Charles anayeshona( kushoto ) mmoja wa mabinti wanaopatiwa mafunzo ya kujitegemeaa katika kituo cha “Mabinti”akijadiliana jambo na maofisa toka Vodocom Tanzania Gloria Mtui na Veronica Rovegno (kulia) wakati Maafisa hao walipowatembelea kituo hicho kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam , kituo kinafadhiliwa na Vodacom Foundation na kinalenga mabinti waliotibiwa ugonjwa wa Fistula na kupona katika hospitali ya CCRBT.





Baadhi ya wanawake wa kituo cha”Mabinti” waliotibiwa Fistula katika hospitali ya CCBRT wakifanya kazi za sanaa za mikono kwa lengo la kujiajiri sambamba na kujikwamua na wimbi la umasikini, Kituo hicho kinachofadhiliwa na Vodacom Foundation kinawawezesha mabinti hao kupata elimu ya kazi za mikono ili waweze kujikimu kimaisha pindi wanaporudi makwao.
Roda George wa kituo cha”Mabinti”alietibiwa Fistula katika hospitali ya CCBRT(kushoto) akiwaelezea jambo kwa vitendo maofisa wa Vodacom Tanzania,Gloria Mtui(katikati)na Reenu Verma walipotembelea kituoni hapo kujionea shughuli mbalimbali za sanaa za mikono zinazofanywa na wasichana wa kituo hicho kinachofadhiliwa na Vodacom Foundation kwa lengo la kuwasaidia wakina mama hao kufunza na kujiajiri sambamba na kujikwamua na wimbi la umasikini na kimaisha pindi wanaporudi makwao.


Wanawake waliopona Fistula CCBRT wapatiwa ujuzi wa kujiajiri Wanawake waliougua  kutibiwa na hatimaye kupona maradhi ya fistula katika Hospitali ya CCBRT iliyopo Dar es Salaam wameamua kujikita katika sanaa ya kazi za mikono kwa lengo la kujiajiri sambamba na kujikwamua na wimbi la umasikini. 

Takribani wanawake wapatao 62, chini ya mpango madhubuti ulioratibiwa na hospitali ya CCBRT, wamekuwa wakihitimu mafunzo mbalimbali ya kazi za mikono zikiwemo sanaa za ushonaji wa batiki, nguo za aina tofauti, utengenezaji wa mabegi, kofia, ususi na kadhalika, katika Kituo kinachoendeshwa na hospitali hiyo kijulikanacho kama ‘Mabinti’ tangu mwaka 2007. 

Akizungumza mbele ya ujumbe wa wadhamini waliotembelea kituo hicho kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mratibu wa Kituo hicho, Katia Geurts, alisema kituo hicho kinatoa mafunzo mahsusi kwa wakinamama waliopona baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa fistula.

“Wengi wao wanatoka katika familia duni, hivyo mafunzo haya wanayoyapata baada ya kumaliza matibabu ya Fistula yanakwenda kuwasaidia kujiajiri wao wenyewe jambo linalowasaidia kupunguza ukali wa maisha,” alisema Geurts.

Aliongeza kuwa baada ya kuhitimu mafunzo hayo kituo hicho huwapatia vyeti vya uhitimu vinavyotambulika, sanjari na vitendea kazi vinavyoendana na stadi stahiki aliyohitimu mwanafunzi kwa minajiri ya kuwarahisishia upatikanaji wa mahitaji muhimu ya maisha yao.

Nae Mkufunzi wa Kituo hicho ambaye awali alikuwa mmoja wa waathirika wa ugonjwa wa fistula hospitalini hapo, Kwenge Charles alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aanze kufundisha wenzake kituoni hapo amebaini kuna idadi kubwa ya wanawake wenye matatizo ya fistula ndani ya jamii lakini waume zao wamekuwa wakiwaficha kwa dhana ya kufisha aibu.

“Kuna haja kubwa ya kuelimisha akinababa wawaruhusu wake zao wenye matatizo waje kutibiwa. Tatizo hili  linatibika na wala sio wa kulogwa kama wengi wanavyodhani, sisi sote hapa kwenye kituo cha mabinti tulikuwa na maradhi hayo na sasa tumepona kabisa wanawake jitokezeni,” alisema  Charles.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha  Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania,Rosalynn Mworia  baada ya kukagua shughuli mbalimbali za mafunzo zinazoendelea kituoni hapo, alisema kwa niaba ya wafanyakazi wa Vodacom Foundatio na Vodafone duniani kote, wataendelea kuwasaidia akinamama wote wanaopatwa na maradhi ya fistula hatua kwa hatua, sanjari na kuhakikisha wanazidisha kasi katika kampeni inayoendelea dhidi ya maradhi hayo.

“Tutaendelea kuwa karibu zaidi na waathirika wa fistula kuanzia hatua ya kuwasafirisha kutoka vijijini na mikoani kwa kuwatumia fedha kupitia huduma yetu ya M-Pesa, pia tutakuwa pamoja wakati wote wa matibabu na baada ya kupona tutawaunga mkono kwenye mafunzo kama haya ili kuwaletea ustawi ulio bora kwa maisha bora kwa ajili yao na familia zao,” alisema Mworia.

No comments

Powered by Blogger.