OLE NASHA AJIVUNIA KUFUTWA KWA BAADHI YA KODI NA TOZO KATIKA SEKTA NDOGO YA MAZAO

 Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe William Tate Ole Nasha (Mb) akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tizeba wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima - Nanenane, mwaka 2017 katika viwanja vya maonesho ya kilimo ya Ngongo Mkoa wa lindi, jana tarehe 1/8/2017. (Picha zote na Mathias Canal)
 Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe William Tate Ole Nasha (Mb) alipotembelea banda la JKT kujionea namna ya uzalishaji mali unaofanywa na Jeshi hilo wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima - Nanenane, mwaka 2017 katika viwanja vya maonesho ya kilimo wa Ngongo Mkoa wa lindi, jana tarehe 1/8/2017.
 Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe William Tate Ole Nasha (Mb) (kulia) akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhandisi Methew J. Mtigumwe wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima - Nanenane, mwaka 2017 katika viwanja vya maonesho ya kilimo wa Ngongo Mkoa wa lindi, jana tarehe 1/8/2017.
Na Mathias Canal, Lindi 

Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Wiliam Tate Ole Nasha (Mb) amesema kuwa kwa muda mrefu serikali imekuwa ikipata malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali hususani kwa wakulima nchini Tanzania wakipinga kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa kwani zimekuwa zikiwanyonya badala ya kuwakwamua na wimbi kubwa la umasikini.

Ameyasema hayo jana tarehe 01/08/2017 wakati akizungumza na wakulima wadau wa kilimo Mifugo na Uvuvi na wananchi kwa ujumla wakati wa uzinduzi wa sikukuu ya wakulima – nane nane, Maonesho yenye kauli mbiu ya “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati” yanayofanyika Kitaifa kwenye uwanja wa maonesho ya kilimo wa Ngongo Mkoani Lindi. 



Alisema kuwa kutokana na malalamiko hayo Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli aliamua kufuta baadhi ya kodi na tozo katika sekta ndogondogo za mazao ili kuibua tija ya uwajibikaji na ukuzaji wa uchumi.

Alisema Jumla ya tozo 80 kati ya tozo 139 zimefutwa na tozo nne (4) zimepunguzwa viwango. Tozo, kodi na ada zinajumuisha kufutwa kwa tozo kumi (10) na mbili (2) kupunguza viwango kwenye zao la tumbaku. Kwenye zao la kahawa zimefutwa tozo 17 na moja (1) kupunguzwa kiwango; sukari zimefutwa 16; pamba tozo zilizofutwa ni mbili (2); kwenye korosho tozo mbili zimefutwa na chai imefutwa tozo moja (1).

Katika kuongeza upatikanaji wa pembejeo tozo tatu (3) zimefutwa na moja (1) imepunguzwa kiwango kwenye mbolea na tozo saba (7) zilizokuwa kwenye mbegu nazo zimefutwa. Katika Ushirika jumla ya tozo 20 zimefutwa katika ngazi mbalimbali.

Alisema kuwa katika Mifugo; kodi, ada na tozo saba (7) ambazo zilikuwa kero kwa Wafugaji, Wafanyabiashara na Wawekezaji nazo zilifutwa na kubakiza zile tu zenye uhusiano wa moja kwa moja katika uendelezaji wa Sekta ya Mifugo. Tozo zilizofutwa zinajumuisha mbili (2) kwenye maziwa; nyama tozo nne (4) na moja (1) kwenye afya ya mifugo.

Katika Uvuvi, jumla ya kodi, ada na tozo tano (5) ambazo ni kero kwa Wavuvi, Wafugaji wa viumbe kwenye maji na wawekezaji nazo zimefutwa.

Alisema kuwa Serikali itaendelea kuchambua kwa kina tozo, ushuru na ada mbalimbali zilizobaki katika kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuangalia uhalali wa kuwepo kwake ili kuwapunguzia wakulima, wafugaji na wavuvi mzigo wa tozo, ushuru na ada zisizokuwa na tija.

‘‘Serikali pia imechukua hatua za makusudi kupunguza ushuru wa mazao uliokuwa unatozwa na Serikali za mitaa kutoka asilimia 5 hadi asilimia 3 kwa mazao ya biashara na kufikia asilimia 2 kwa mazao ya chakula. Vile vile, Serikali imezielekeza Serikali za Mitaa kuacha kutoza ushuru kwa wazao yanayosafirishwa halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine yenye uzito usiozidi tani moja (1)’’ Alisema Mhe Nasha

Aliongeza kuwa Hatua nyingine iliyochukuliwa ni ya kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye vyakula vya mifugo vinavyotengenezwa hapa nchini ili kupunguza gharama ya kununua chakula hicho kwa Wafugaji. Serikali pia, imesamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye mayai ya kutotoleshea vifaranga, lengo likiwa ni kupunguza gharama ya uzalishaji vifaranga na kukuza Sekta ndogo ya Ufugaji ili iweze kuongeza mchango katika Pato la Taifa.

Mhe Nasha alisema kuwa Kuanzia msimu huu wa kilimo Wakulima wa korosho watapata bure pembejeo aina ya salfa zilizokuwa zikiuzwa kwa bei ya ruzuku.
 

Hatua hiyo ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa vikwazo vyote vilivyokuwa vinawakabili wakulima wa zao la korosho vinaondolewa ili waongeze uzalishaji na tija zaidi kutokana na zao hilo.

Aidha alisema kuwa Serikali itaendelea kuhimiza matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Mfumo huu umesaidia kupanda kwa bei ya korosho na mapato kwa wakulima kupitia vyama vikuu vya ushirika vya TANECU, MAMCU, RUNALI, Lindi Mwambao, TAMCU na CORECU.

Alisema wakulima na wafanyabiashara Wote ni mashahidi kuwa katika msimu wa ununuzi uliopita wa mwaka 2016/2017 vyama hivyo viliuza korosho na kuwalipa wakulima jumla ya Shilingi bilioni 809.18 ikilinganishwa na malipo ya Shilingi bilioni 293.09 msimu wa 2015/2016. Kiasi hiki cha fedha ni kikubwa na ni mafanikio makubwa ambayo ni ya kujivunia.

No comments

Powered by Blogger.