RONALDO ANAFYATUA TU!


                      Akiongea jambo na lafiki yake huku akiwa na familia yake.

MIEZI kadhaa iliyopita, Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli aliwahi kunukuliwa akisema kuwa kwa jinsi serikali yake inavyofanya kazi, ikiwemo kutoa elimu bure, akawapa ruhusa wanandoa kuendelea kutafuta watoto ambapo alitumia neno kufyatua.
Neno hilo limekuwa maarufu kutokana na alivyolitumia kiongozi huyo, hivyo kwa mwenendo wa sasa unavyoelekea kwa mshambuliaji staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ni kama ameamua kufyatua tu katika suala la kutafuta watoto.
Akiwa na umri wa miaka 32, kwa sasa ni baba wa watoto watatu, wawili akiwa amewapata mwaka huu na anatarajiwa kumpata wa nne baadaye mwaka huu.
                                                       Akiwa kamshika mpenzi wake.

Inakumbukwa kuwa, mtoto wake wa kwanza anayejulikana kwa jina la Cristiano Jr mwenye umri wa miaka saba, alizaliwa Juni 2010 huku mama yake akiwa hajulikani kwa mashabiki wa mchezaji huyo.
Ndivyo ilivyokuwa kwa pacha wake wa mwaka huu ambao ni Eva na Mateo, nao wamezaliwa nchini Marekani kama ilivyokuwa kwa kaka yao huku Ronaldo akiwa mgumu kutaja mama wa watoto hao.
Kuelekea kumpata mtoto wake wa nne, ameamua kubadili staili kutoka ya usiri wa mama mtu na sasa mtoto huyo anatarajiwa kupatikana kupitia kwa mchumba wake, Georgina Rodriguez ambaye ana ujauzito.
Ronaldo alithibitisha juu ya ujauzito huo juzi baada ya kuwepo kwa tetesi nyingi kuwa mrembo huyo ni mama kijacho. Staa huyo wa Madrid ambaye ni raia wa Ureno, alithibitisha kwa kukiri kuwa ni kweli na anafuraha kumsubiri mwanaye huyo.
Georgina, 23, amekuwa akionekana maeneo tofauti huku ‘kitumbo’ kikiwa kimetuna ambapo mama yake Ronaldo aliwahi kukana kuwa mkwewe huyo siyo mjamzito.
                                                   Akiongozana na mpenzi wake.
 Walipoanzia
Kabla ya kukutana na Ronaldo, Georgina alikuwa ni mfanyakazi wa maduka ya Gucci kwenye Jiji la Madrid.
Akiwa katika pitapita zake za masuala ya mitindo, ndipo Ronaldo alipokutana na mrembo huyo kwenye tamasha moja la maonyesho ya mavazi.
Wakiwa huko, ndipo walipobadilishana namba na kuanza kuwasiliana, uhusiano wao ulianza kwa siri kabla ya baadaye kunaswa wakiwa pamoja nchini Ufaransa.
Haijajulikana uhusiano wao ulianza lini hasa lakini mara ya kwanza wanaonekana hadharani pamoja ilikuwa Novemba, 2016.
Anakubalika na familia
Licha ya kujulikana wazi kuwa Ronaldo ametokea kwenye familia ya kimasikini, alipambana na kupata utajiri mkubwa, baada ya miaka mingi ya kufanya starehe huku akifanya kazi ambapo miradi mingi ilikuwa ikisimamiwa na mama na dada yake, inavyoonekana sasa anahitaji mke na watoto kwa ajili ya kuendeleza familia na utajiri wake.
Awali ilionekana bado hajapata mwanamke sahihi na ndiyo maana hata aina ya utafutaji wa mtoto wake wa kwanza na hawa wawili aliowapata mwaka huu aliufanya kwa kificho huku mama zao wakiwa hawajulikani.
Kitendo cha kumtambulisha Georgina kinamaanisha kuwa amemkubali na kuna tetesi kuwa wawili hao wanaweza kufikiria juu ya kufunga ndoa baada ya kujifungua.

    Mshambuliaji staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo akiwa na familia yake.

Kuonyesha anamkubali, wiki kadhaa zilizopita Ronaldo alipiga picha akiwa na familia yake pamoja na ndugu zake wengi wakiwa pamoja wanaogelea kwenye bwawa la nyumbani kwa mchezaji huyo.
Licha ya kuwa mama wa watoto watatu wa sasa wa Ronaldo hawajulikani, lakini Georgina amekuwa akionekana kuwa pamoja na watoto hao kama vile yeye ndiye mama watoto.
Kuhusu mama wa watoto wake, Ronaldo aliwahi kunukuliwa akisema: “Kwa makubaliano niliyonayo, kuhusu mama hilo litabaki kuwa siri kwa watoto wangu.”
Wakati timu ya Real Madrid ikiwa imeshaanza mazoezi kujiandaa kwa msimu ujao, kwa sasa Ronaldo ana muda mwingi wa kuwa na familia yake hiyo kwa kuwa yupo katika mapumziko baada ya kumalizika kwa msimu wa 2016/17 kisha akaenda kuitumikia Ureno kwenye michuano ya Kombe la Mabara.

No comments

Powered by Blogger.