Yanga, SportPesa Kusaini Mkataba Mnono Kesho Jumatano

                                                             Kikosi cha timu ya Yanga.
Baada ya kusaini mkataba na Simba, sasa Kampuni ya SportPesa inatarajiwa kusaini mkataba na Klabu ya Yanga, kesho Jumatano.
Awali kulikuwa na taarifa kuwa mkataba huo ambao ulikuwa usainiwe tangu wiki iliyopita, ilipangwa usainiwe leo Jumanne wakati Yanga ikicheza dhidi ya Toto Africans katika Ligi Kuu ya Vodacom lakini kutokana na mambo kadhaa kutokuwa sawa ikabidi ipangwe kesho Jumatano.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa kila kitu kimekamilisha na mkataba huo wa Yanga na kampuni hiyo ya Sportpesa sasa utasainiwa kiroho safi baada ya pande zote kukubaliana.
Pamoja na hivyo habari kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa dili lao lina thamani kubwa kiasi kuliko lile la Simba ambalo lina thamani ya shilingi bilioni 4.9.
Katika mkataba huo wa Simba, klabu hiyo itapokea shilingi milioni 888 katika mwaka wa kwanza huku kukiwa na ongezeko la asilimia tano kwa kila mwaka katika miaka mitano ya mkataba huo.
Kama hivyo haitoshi, Simba imepewa motisha iwapo watachukua ubingwa wa ligi kuu watapewa shilingi milioni 100 Huku Sportpesa wakitenga shilingi milioni 250 iwapo Simba wakibeba Kombe la Kagame au michuano iliyo chini ya Caf.
Hivyo Wanayanga wanasubiri kwa hamu juu ya mkababa huo ambao ulisababisha kuibuka kwa mgogoro mzito wa kiuongozi. Ikumbukwe kuwa katika miezi ya hivi karibuni Yanga imekuwa ikipitia kipindi kigumu kutokana na mwenyekiti wake Yusuf Manji kuwa na matatizo binafsi na hivyo kutokuwa karibu na klabu ambapo yeye ndiye amekuwa akitoa msaada mkubwa wa fedha.


No comments

Powered by Blogger.