Zitto Kabwe: Sitta Amenilea kwa Kunisomesha
Alfajiri ya tarehe 7 Novemba
2016, tunaamka na kukutana na habari za kusikitisha kuwa Mzee Samwel
John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ametangulia mbele ya haki. Babu alikuwa mgonjwa kwa kitambo kidogo
akisumbuliwa na saratani ya tezi dume.
Majonzi ni makubwa kwa Taifa kutokana
na sababu kubwa kwamba Samwel John Sitta alitumikia nchi yetu kwa muda
mrefu na kwa uadilifu mkubwa.
Sisi wengine pia kwa kiasi fulani
kukua kwetu kisiasa kumetokana na utumishi wake uliotukuka kwa nchi yetu
alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika
tanzia hii ninamkumbuka Mzee Sitta Kwa namna nilivyofahamiana naye
binafsi na namna nilivyomshuhudia katika kazi zake.
Sitta ananigusa mimi binafsi moja kwa
moja. Alikuwa babu yangu. Tukiwa bungeni akiniandikia kitu alikuwa
akitumia neno hilo “babu” kwa mwandiko wake mzuri usiotoka kwenye
kumbukumbu zangu kabisa.
Aliniapisha kiapo cha ubunge Desemba
29, 2005. Maneno ambayo aliniambia baada ya kunikabidhi Kanuni za Bunge
na Katiba ya Nchi niliyaandika kwenye daftari langu la kumbukumbu siku
hiyo hiyo jioni.
Baada ya kula kiapo cha utii na cha
uaminifu kawaida wabunge hupewa mkono na mwapishaji na kupewa nyaraka za
kazi. Kwa upande wangu Mzee Sitta alinikumbatia na kuniambia, “utakuwa
kiongozi muhimu sana kwa nchi yetu. You have a bright future.”
Maneno haya hayajawahi kutoka katika
kumbukumbu zangu na kila nikipata misukosuko yangu kisiasa huyakumbuka
na wakati mwingine yeye mwenyewe alikuwa akinipigia na kunikumbusha na
kunitia moyo. Babu alikuwa mlezi wa wanasiasa vijana.
Sitta pia amenilea kwa kunisomesha.
Mwaka 1996 nilikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Galanos jijini
Tanga nikisomea mchepuo wa Historia, Jiografia na Uchumi (HGE).
Hali ya hewa ya Tanga haikunipenda,
hivyo nikawa naumwaumwa sana. Pia nilitaka kusoma Hesabu badala ya
Historia. Wakati wa likizo ya Desemba mwaka 1996, nilitoka Tanga
nikaenda Dar es Salaam, Wizara ya Elimu kuomba uhamisho kwenda shule
yenye Somo la Hesabu, kidato cha Tano na Sita. Nikakataliwa. Lakini
nikaambiwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari wakati huo Bwana Ndeki
alisoma na Samwel Sitta.
Kipindi hicho Mzee Sitta akiwa
Mkurugenzi wa Investments Promotion Centre (IPC) kabla haijabadilishwa
jina kuwa Tanzania Investments Centre (TIC). Nikaenda Ofisi za IPC
mahali ambapo leo ni CRDB Tawi la Azikiwe.
Nilipofika Katibu Muhtasi wake
akaniuliza kama nina miadi na bosi wake, nikasema hapana. Akaniambia
hawezi kukuona. Nikasisitiza sana na kumlilia dada yule aniruhusu dakika
chache tu. Akaniruhusu.
Nilipofika Mzee Sitta aliniuliza shida
zangu kwa heshima kubwa. Nikamwambia kwamba ninataka kuhama shule.
Akaniomba matokeo yangu ya Kidato cha Nne, nikampa maana nilikuwa
natembea nayo. Alipoyasoma akaniambia, “wewe hupaswi kuhangaika kutafuta
shule maana kwa matokeo yako unaweza kusoma shule yoyote nchini ya
chaguo lako”. Akainua simu akampigia Bwana Ndeki. Kisha akaniandikia
kikaratasi niende wizarani muda uleule. Nilipofika wizarani nikapewa
uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mazengo.
Nilipotoka nje ya wizara nikakutana na
kijana mwingine anaomba uhamisho, yeye anatoka Mazengo anataka kwenda
Tosamaganga, Iringa. Akaniambia, achana na Mazengo hakuna mwalimu wa
Uchumi na hali ya vyoo ni mbaya sana. Nikarudi kwa Mkurugenzi. Mzee
aliyenipa uhamisho aliponiona narudi na kumwambia sitaki Mazengo
akachukua fomu zangu za uhamisho na akachukua ‘whiteout’ akafuta Mazengo
na kuweka Tosamaganga huku akisema kwa hasira “ nyie watoto wa wakubwa
bwana”. Sikujali nikaenda zangu Tosamaganga kusoma Economics, Geography
na Mathematics (EGM).
Sitta akaendelea kufuatilia maendeleo
yangu shuleni na baadaye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya
InWent nchini Ujerumani.
Nilipotoka Ujerumani kusoma masomo ya
Juu ya Biashara ya Kimataifa mwaka 2004 ilipaswa niwe na mradi wa
kitaaluma. Nikachagua kuunganisha kampuni za Kijerumani na Tanzania kwa
kuandika mradi wa kuchukua wafanyabiashiara 20 kutoka Tanzania na
kuwaunganisha na wengine 20 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Ilibidi kupata Taasisi ya Tanzania kwa
ajili mradi huo na Mzee Sitta akawa mstari wa mbele kuhakikisha mradi
unafanikiwa na tukautekeleza kwa umakini kwa msaada wa ofisa wa TIC
aitwaye Phina Lyimo.
Mwaka mmoja baadaye tukakutana na Mzee
Sitta bungeni, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki na mimi
nikiwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Ulezi wake ukaendelea mpaka
mauti yalipomkuta leo mapema asubuhi (jana). Nimempoteza babu mlezi.
Sitta alikuwa mwana mageuzi (reformer)
na kupitia uanamageuzi wake alifanya mabadiliko makubwa sana katika
uendeshaji wa shughuli za Bunge. Sisi tuliohudumu kwenye Bunge la Tisa,
tukimwita Spika wa Viwango na Kasi, tuliona wenyewe juhudi zake za
kuliweka Bunge katika nafasi yake ya Kikatiba. Licha ya kuhakikisha kuwa
maslahi ya Wabunge yanalingana na hadhi ya Bunge, alihakikisha pia kuwa
Bunge linaisimamia Serikali sawa sawa. Haikuwa kazi rahisi sana kwani
kulikuwa na mvutano mkubwa sana kati ya Spika Sitta na Waziri Mkuu
Edward Lowasa katika kuleta mabadiliko hayo.
Tulikuwa tunaambiwa kuwa mvutano huo
ulitokana na tetesi kwamba Sitta ndiye alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa
Tanzania na hivyo kuwa na msuguano na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo.
Si Sitta wala Lowasa ambaye alithibitisha ama kukanusha tetesi hizo.
Sitta ametangulia mbele ya haki, labda Edward Lowasa ataweza kusemea
hili siku za usoni.
Sitta alitumia fursa ya msuguano huo
kufanya mabadiliko makubwa ya kanuni za Bunge na kutoa uhuru mpana wa
mawazo ndani ya Bunge na kuhakikisha kuwa taarifa za Kamati za Bunge na
hususani Kamati za Usimamizi wa Serikali zinasomwa na kujadiliwa ndani
ya Bunge kwa mujibu wa Kanuni.
Wakati wa Bunge la Nane, Taarifa za
CAG hazikuwahi kusomwa hata mara moja. Ni kutokana na mabadiliko haya ya
kanuni ndipo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (Poac )
ilianzishwa Machi, mwaka 2008.
Nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
kwanza wa kamati hiyo na kuingia kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge
ambayo kipindi hicho tuliiona kama kamati ya wabunge wazee. Namna
nilivyoingia kuwa Mwenyekiti wa Poac nayo ni hadithi nyingine ya namna
ya malezi ya kiuongozi yaliyofanywa na Spika Sitta.
Sikuwa nimejaza fomu kuomba Kamati ya
Poac. Wakati huo ulikuwa ni wakati wa vuguvugu la Buzwagi (Mkataba wa
Madini uliosainiwa na Waziri wa Nishati hotelini nchini Uingereza kwa
siri ). Nilikuwa mjini Bagamoyo kwenye kazi za Kamati ya Bomani nikiwa
na Harrison Mwakyembe na Ezekiel Maige.
Spika wa Bunge akanipigia simu,
akaniambia “Babu, kesho kuna uchaguzi wa Kamati za Bunge. Nimekuteua
Kamati ya Poac ambayo ni kamati mpya itakayokuwa chini ya Kambi ya
Upinzani. Najua hukuomba kuwa mjumbe wa kamati hii, lakini nahitaji damu
changa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge. Naomba unikubalie na kesho
uwepo Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi na ugombee. Utashinda maana
nimeshafanya kazi yangu”. Sikuwa na namna ya kukataa japo nilitaka sana
kuendelea kuwa Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya Abdallah Kigoda, ama
Kamati ya Nishati na Madini chini ya Mzee William Shelukindo.
Ombi la Mzee ni amri. Nikawa
Mwenyektii wa Poac na kuwa mmoja wa washauri wakuu wa Spika wa Bunge.
Kamati ya PAC ikawa chini ya Mzee John Cheyo na Kamati ya Laac ikawa
chini ya Dk Wilibrod Slaa. Ilikuwa ni Bunge lenye meno kweli kweli.
Spika Sitta alikuwa mbabe. Ubabe wake
ulimsababisha kufanya maamuzi ambayo wakati mwingine yalimweka kwenye
matatizo na wananchi. Mfano mzuri ni suala la Hoja Binafsi ya Buzwagi na
Hoja ya Wizi wa Fedha Benki Kuu ( Epa). Mwanzoni, Spika alikuwa upande
wa wabunge wenye hoja hiyo yaani mimi na Dk Slaa kiasi cha kuziboresha
hoja zile kwa kalamu yake mwenyewe. Wabunge wa chama chake hawakuwa
wanapenda hoja hizi na hivyo Waziri Mkuu Lowasa akamweka kwenye wakati
mgumu sana wa kuegemea upande wa Serikali. Hoja ya Dk Slaa akaitupa kuwa
‘ ni makaratasi ya kuokoteza’. Hoja yangu akaiingiza bungeni na
akasimamia kusimamishwa kwangu bungeni. Wananchi walimkasirikia sana.
Siku moja usiku, nikiwa nyumbani kwa
Freeman Mbowe Mikocheni, Sitta akanipigia simu kulalamika kuwa wafuasi
wangu wanamtukana kwa meseji. Akaniambia niwakataze. Nilimkubalia tu,
lakini sikuwa na uwezo huo. Nchi ilikuwa imevimba. Ilikuwa Oktoba 2007,
Sitta alijua namna ya kusoma nchi na kuwapa watakacho, wakati mwingine.
Mwezi Novemba, katika kujibu kiu ya wananchi kuhusu uwajibikaji na
kufuta makosa ya Buzwagi na Epa, Spika alisimamia kuundwa kwa Kamati
Teule kuchunguza suala la Mkataba wa Richmond. Yaliyofuata yalikuwa
historia. Taarifa ya Kamati Teule ilisababisha ‘kuanguka’ kwa Serikali
kwa mara ya kwanza katika hsitoria ya Tanzania, Waziri Mkuu Lowasa
alilazimika kujiuzulu ndani ya Bunge, Baraza la Mawaziri likavunjika na
Serikali mpya kuundwa chini ya Mizengo Kayanza Pinda.
Spika Samwel Sitta akawa ni Spika
pekee wa nchi yetu aliyeshuhudia uundwaji wa Serikali mbili ndani ya
miaka mitano ya uspika wake. Mzee Msekwa yeye alikaa miaka 10 na Waziri
Mkuu mmoja, ingawa mwaka 1993-1995 naye aliona mabadiliko ya mawaziri
wakuu, kutoka John Malecela kwenda kwa Cleopa Msuya. Baada ya kujiuzulu
kwa Lowasa, Samwel Sitta hakurudi nyuma tena. Aliendelea kuwa Spika wa
Viwango mpaka alipomaliza muda wake katika Bunge la Tisa.
Spika Sitta alikuwa mwepesi kuomba
msamaha alipokosea. Nakumbuka siku moja mwaka 2009 alimfukuza bungeni
mzee mwenzake John Cheyo kwa makosa ambayo Cheyo hakufanya. Baadhi yetu
tukakasirishwa sana na kitendo kile. Nikaenda kumwona Mzee Sitta ofisini
kumwuliza kulikoni amdhalilishe mwenzake namna ile. Akanieleza kuwa
hakuwa sawa na atamwomba radhi John Cheyo. Tukiwa kwenye Kamati ya
Uongozi ya Bunge kwa ajenda za kawaida tu, Mzee Sitta akamwomba radhi
Mzee Cheyo.
Nikikumbuka kisa hiki nacheka sana
maana Jaji Werema aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alicheka mpaka
kuanguka chini. Sababu? Mzee Sitta aliketi kwenye kiti chake, wenyeviti
wote wa kamati tukiwa tumetulia tuanze kikao. Mzee Sitta akasema, “John,
naomba radhi kwa tukio lililotokea bungeni wiki iliyopita. Sijui
nilikuwa nina nini siku hiyo, nadhani nilisumbuliwa na watu
wanaopitapita jimboni kutaka kunitoa, nisamehe mzee mwenzangu”. Kicheko
ukumbi mzima na Cheyo akamkubalia radhi yake huku naye akicheka na
yakaishia hapo. Wazee hawa wawili wameandika pamoja kitabu, ‘Bunge lenye
Meno.’
Nimwelezeje zaidi Babu? Nimwelezeje
zaidi Spika wa Kasi na Viwango Samwel Sitta? Mwanasiasa shupavu, jasiri,
mwenye ngozi ngumu, mbabe, mnyeyekevu inapobidi na mwenye uthubutu.
Tangulia Babu. Tangulia Mtemi wa Unyanyembe Samwel John Sitta. Umeondoka
duniani lakini bado unaishi kupitia kazi zako kwa nchi yetu.
Mwandishi wa makala haya ni Kiongozi wa ACT- Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini.
Post a Comment