Vyeti FEKI vya vifo Vyatumika Kupata mikopo Elimu ya Juu
Bodi ya
Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imebaini kuwepo kwa baadhi ya wanafunzi
ambao wamewasilisha vyeti feki vya vifo vya wazazi wao ili waonekane
kama ni watoto yatima; hivyo wapewe kipaumbele cha kupatiwa mkopo.
Kuwepo
kwa vyeti hivyo vya bandia kumegunduliwa na bodi hiyo baada ya kupeleka
nakala za vyeti vyote vya vifo ofisi ya Msajili wa Vizazi na Vifo
(Rita) kwa ajili ya uthibitisho ndipo ikagundulika kuwepo kwa kasoro
hizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul- Razaq Badru, amesema
kuwa wahusika wote ambao wamewasilisha vyeti hivyo feki suala lao
limekabidhiwa kwa mamlaka zinazoshughulika na makosa ya jinai.
Hata hivyo, Badru hakutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo kwa maelezo kuwa bado wanaendelea na ukaguzi.
“Bado tunaendelea kuchunguza na idadi yao hapa sina, tukikamilisha tutawaita kuwaambia idadi yao,”
alisema Badru na kuongeza kuwa kutokana na kasoro hizo, ndio maana kuna
baadhi ya watu wanaolalamika kuwa ni yatima, lakini hawakupata mkopo.
“Hayo malalamiko ya kwamba kuna yatima wamekosa mikopo tumeyasikia, lakini na sisi tunajiridhisha kuwa huyu ni yatima baada ya kupata uthibitisho wa vyeti vya vifo kutoka Rita,” alisema Badru.
“Hayo malalamiko ya kwamba kuna yatima wamekosa mikopo tumeyasikia, lakini na sisi tunajiridhisha kuwa huyu ni yatima baada ya kupata uthibitisho wa vyeti vya vifo kutoka Rita,” alisema Badru.
Aliongeza
kuwa hata wale ambao ni wanafunzi wenye ulemavu, bodi hiyo haiwezi
kuwaamini kama ni walemavu, bali hadi wapate uthibitisho kutoka kwa
daktari wa wilaya (DMO) kuthibitisha ulemavu wa mwombaji.
Alisema
baadhi ya wanafunzi ambao wanalalamika kuwa wamekosa mikopo ni wale
ambao maombi yao yalikaguliwa na kukutwa na dosari kadhaa, na wakaombwa
wazirekebishe kasoro hizo, lakini baadhi yao hawakufanya hivyo.
Badru
alisema bodi yake baada ya kuchambua maombi ya waombaji wote; hadi sasa
imeshatoa mikopo kwa wanafunzi wote wanaostahili wakiwemo yatima,
walemavu, wanafunzi wanaosoma kozi za kipaumbele na wahitaji wanaosoma
kozi zingine.
Akizungumzia
suala la baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambao
wamekosa mikopo na kulazimika kurudi makwao, Badru alisema wanafunzi hao
yawezekana ni miongoni mwa wale ambao hawakukidhi vigezo vya kuweza
kupewa mkopo.
“Pale
Dodoma tumetoa mkopo kwa wanafunzi wapya takribani 3,000, hivyo hao
wanaoondoka kurudi nyumbani yawezekana wako kwenye kundi la wanafunzi
ambao hawakukidhi vigezo vya kupewa mkopo,” alisema Badru.
Alisema
sio rahisi kutoa mkopo kwa wanafunzi wote, kwani Serikal inaendeshwa
kwa bajeti na mwaka huu wamechagua kusomesha wanafunzi 25,000 kulingana
na bajeti iliyopo pamoja na kulingana na mahitaji ya wataalamu
wanaotakiwa na kutokana na vipaumbele vyake.
Alisema anatambua kuna wanafunzi zaidi ya 10,000 ambao wamekosa mikopo na kuongeza; “lakini
bajeti ya mwaka huu imeishia hapo, mwaka kesho tunaweza kuishauri
Serikali iongeze fedha baada ya kuwa tumefanya tathmini uhitaji wa
mikopo hiyo.”
Hata
hivyo, Badru alisema kuna wanafunzi ambao wanasoma kozi za kipaumbele,
lakini wazazi wao wana uwezo, hao nao hawakupatiwa mikopo licha ya kuwa
kwenye kundi la wanaostahili mkopo.
“Kuna
mtu anasomea udaktari, lakini wazazi wake wana uwezo, na kuna
mwanafunzi anasomea sayansi ya jamii na wazazi wake ni watu wasio na
uwezo, hapo lazima tuangalie mhitaji ni yupi kati ya hao wawili na ndiye
tunampatia mkopo,” alisema Badru.
Alisema
kuna wanafunzi wanasoma kozi za kipaumbele baadhi yao hawakupata mkopo
kabisa na baadhi yao wamepatiwa mkopo kidogo baada ya bodi hiyo kufanya
tathmini ya hali ya uchumi ya wazazi au walezi wa mwombaji.
Post a Comment