Rais Magufuli na Rais Kenyatta Wazindua Barabara ya Southern By-Pass
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe.
Uhuru Kenyatta leo tarehe 01 Novemba, 2016 wamezindua barabara ya
Southern By-pass iliyojengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari
katika Jiji la Nairobi nchini Kenya.
Sherehe za uzinduzi wa barabara ya Southern By-pass zimehudhuriwa na Naibu Rais wa Kenya Mhe. William Ruto.
Sherehe ya uzinduzi wa barabara hiyo
yenye urefu wa kilometa 28 na inayounganisha maeneo mbalimbali ya Jiji
la Nairobi imefanyika katika eneo la Karen nje kidogo ya Jiji la
Nairobi.
Akizungumza katika sherehe hiyo Rais
Magufuli amempongeza Rais Kenyatta na Serikali yake kwa kujenga barabara
hiyo ambayo sio tu itawasaidia wananchi wa Kenya bali pia itawasaidia
wananchi wa Afrika Mashariki wanaotumia barabara zinazopitia Nairobi.
Rais Magufuli pia ameishukuru Serikali
ya China kupitia benki yake ya Exim ambayo imetoa mkopo wa kujenga
barabara hiyo, kwa kuendelea kuziamini nchi za Afrika Mashariki na
kuzikopesha mikopo inayosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo
ikiwemo ujenzi wa barabara.
“Wananchi wanahitaji maendeleo na haya
ndio maendeleo, barabara hii itasaidia kuinua uchumi na itasaidia
masuala ya kijamii” amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amesema viongozi wa
Afrika Mashariki wameamua kufanya kazi ya kuharakisha maendeleo na
kuinua maisha ya wananchi, na kwamba ili kufanikisha hilo wamedhamiria
kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara zinazounganisha
nchi wanachama na kujenga vituo vya pamoja vya utoaji wa huduma za
mpakani (One Stop Border Post).
Kwa upande wake Rais Kenyatta amesema
kujengwa kwa barabara hiyo kumesaidia kupunguza msongamano wa magari
katika Jiji la Nairobi na pia kutaboresha shughuli za maendeleo ya
wananchi.
Mhe. Kenyatta amemshukuru Rais
Magufuli kwa kuungana nae kuzindua barabara hiyo na amesema Kenya
itaongeza juhudi katika utekelezaji mradi wa ujenzi wa barabara
zinazounganisha Kenya na Tanzania zikiwemo barabara ya Malindi kupitia
Saadani hadi Bagamoyo nchini Tanzania na barabara ya Voi – Taveta-
Horiri-Arusha.
Rais Dkt Magufuli akiangalia usindikaji wa Samli alipotembea kiwanda cha maziwa cha Eldoville nchini Kenya leo.Sherehe za uzinduzi wa barabara ya Southern By-pass zimehudhuriwa na Naibu Rais wa Kenya Mhe. William Ruto.
Kabla ya kuzindua barabara hiyo Rais
Magufuli ametembelea kiwanda kidogo cha kusindika maziwa cha Eldoville
kilichopo katika eneo la Karen ambacho kinamilikiwa na familia ya
mkulima Bw. James Karuga.
Familia hiyo ilianzisha kiwanda cha
kusindika maziwa mwaka 1985 kwa uzalishaji wa chini ya lita 1,000 kwa
siku na hivi sasa imefikia uzalishaji wa lita 5,000 kwa siku na
inatarajia kuongeza uzalishaji hadi lita 70,000 katika mwaka mmoja ujao
baada ya kuongeza kiwanda cha pili.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Nairobi
01 Novemba, 2016
Post a Comment