Bashe adai Lowassa alionewa CCM, aeleza uhusiano wao kwa sasa
Mbunge
wa Nzega, Hussein Bashe (CCM) amesema kuwa anaamini waziri mkuu wa
zamani, Edward Lowassa aliondolewa kwa kuonewa katika mchakato wa
kugombea urais ndani ya CCM.
Bashe
amesema kuwa kitendo hicho alichokiita cha kiuonevu ni changamoto kubwa
ndani ya CCM na kwamba wengi wameonewa katika michakato ya kuwania
nafasi mbalimbali.
“Yaliyomkuta
Lowassa yamewakuta wengi ndani ya CCM, hivyo jambo hilo sio geni,”
Bashe anakaririwa na Mwananchi. “Wapo waliobaki na wapo walioamua kuhama
chama kwa sababu ni binadamu. CCM ina historia hiyo, hii ndiyo
changamoto yake kubwa,” aliongeza.
Mbunge
huyo alifafanua kuwa kwakuwa Lowassa alituhumiwa kwa mengi ndani ya
chama hicho, alipaswa kuitwa na kuelezwa tuhuma zake na sababu za
kuondolewa jina lake ili umma ufahamu.
Alisema
kuwa katika chama hicho, kashfa nyingi hufanywa kwa sababu maalum na
hubuniwa kwa ajili ya kufikia lengo fulani dhidi ya mtu au kikundi cha
watu.
Alisema
kuwa mbali na sakata la Richmond lililopelekea Lowassa kujiuzulu nafasi
ya uwaziri mkuu, masakata ya Lugumi na Tegeta Escrow ni sehemu yale
yaliyobuniwa kwa lengo maalum.
“Tazama
wanavyofunika sakata la Lugumi. Usiende mbali angalia sakata la Escrow.
Tumeadhibu waliopata fedha kutoka benki ya Mkombozi, vipi wa Stanbic?
Wizi mwingine uliofanywa nchi hii una uhusiano kati ya Serikali na
vikundi vya watu wenye uhusiano na Serikali,” Bashe aliliambia
Mwananchi.
Akizungumzia
uhusiano wake na Lowassa ambaye alikuwa anamuunga mkono wakati wa
mchakato wa kugombea urais kupitia CCM, Bashe alisema hivi sasa hawana
uhusiano tena wa urafiki wa kisiasa.
Alisema kuwa alimshauri sana Lowassa kutohama CCM, avumilie, lakini hakufanikiwa kumshawishi, hivyo waliagana.
“Lowassa
ni mzee wangu. Ni mtu ambaye namheshimu na nitaendelea kufanya hivyo,
ingawa kwa sasa hatuna uhusiano wa kisiasa,” alisema.
Lowassa
alihama CCM baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kuwania
urais, alihamia Chadema na kupewa nafasi ya kugombea urais katika
uchaguzi unaotajwa kuwa na ushindani mkali zaidi tangu kuanzishwa kwa
mfumo wa vyama vingi.
Post a Comment