Serikali Yakubali Kurejesha Posho ya Sh. 8500 kwa Siku kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Nchini

Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetuliza hasira za wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kurejesha posho ya chakula na malazi ya Sh8,500 kwa kila mmoja na kwamba tofauti baina yao itakuwa viwango vya ada.

Ufafanuzi huu uliotolewa jana usiku na Waziri wa Elimu, Sayansi , Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumza katika mahojiano maalimu na kituo cha runinga cha Taifa -TBC utakuwa faraja kwa wanafunzi ambao chini ya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) walipanga kushinikiza walipwe posho ya Sh8,500 kwa siku kama ilivyokuwa awali. 
 
Hatua ya wanafunzi kujenga umoja ili kushinikiza haki katika posho ilitokana na baadhi yao kuingiziwa kati ya Sh40,000 na 70,000 badala ya Sh 510,000, hali ambayo ilizua sintofahamu. 
Ndalichako alisema tofauti ya malipo itakuwa katika ada na siyo posho, “Vigezo vya mikopo vimebadilika, kila mwanafunzi atapata fedha tofauti lakini tumefanya marekebisho kwenye posho ya chakula ambayo kila mwanafunzi atalipwa Sh8,500 kama awali.” 
Kwa mujibu wa utaratibu wa Bodi hiyo, malipo hayo ya chakula na malazi hutolewa kila baada ya miezi miwili. 

Mapema jana, Daruso iliwataka wanafunzi wa chuo hicho kutotia saini fomu za fedha za mikopo yao mpaka itakapowapa ruhusa ya kufanya hivyo. 
Rais wa Daruso, Erasmi Leon alisema hayo jana wakati akizungumza na wanafunzi wenzake kuhusu kusudio la kwenda HESLB kwa ajili ya kutafuta haki yao ya msingi. 
“Ninachowasihi tuwe pamoja. Tuwe wamoja na twende pamoja. Tutakwenda wawakilishi kutafuta nafasi kwa amani waweze kusikia tuna hoja gani lakini tukinyimwa hii nafasi tutaenda kuitafuta tukiwa wengi,” alisema na kuongeza:
 “Tuwe watulivu kwa sasa tutakapowahitaji muda na wakati wowote kwa lolote tushirikiane ili twende pamoja tumalize pamoja tuhakikishe tunapata Sh8,500 kwa kila mwanafunzi kwa chakula na malazi,” alisema. 
Kuhusu suala hilo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ulisema wajibu wake ni kupokea na kusambaza majina na taarifa kutoka Bodi kwa wanafunzi. 
Akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi waliofika ofisini kwake kujua hatima yao na waliopata mikopo kuchukua fomu za kutia saini, Ofisa Mikopo wa UDSM, Lugano Mwakyusa alisema wenye jukumu la kujua walio na sifa ya kupata mikopo ni Bodi ya Mikopo. 
“Tunaendelea kupokea majina kutoka bodi. Tayari hapa kuna majina 949 yameshatoka, wengine tuzidi kusubiri na wale mwaka wa pili na tatu ambao walikuwa na mitihani ya marudio taarifa zao zitapelekwa bodi,” Mwakyusa aliwaambia wanafunzi waliokuwa wamejaa ofisini kwake.
 Kulikuwa na hali ya sintofahamu chuoni hapo jana baada ya wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza kuonekana wakiwa wameshika bahasha za kaki zilizokuwa na fomu za usajili wanazotakiwa kujaza huku wakihangaika kutokana na kutojua kiasi cha mkopo. 
Juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, AbdulRazaq Badru alieleza kwamba ingawa wanafunzi 88,000 waliomba mikopo kutoka HESLB, uwezo wa bodi hiyo ni kutoa kwa wanafunzi 21,500 pekee sawa na asilimia 24 na waliokuwa wameshapatiwa walikuwa 11,000 sawa na asilimia 12. 
Takwimu hizi zinaonyesha zaidi ya robo tatu ya wanafunzi wanaohitaji mikopo watakosa kutokana na uwezo mdogo wa kifedha.

No comments

Powered by Blogger.