Ithan Mahafudh: Mtoto wa miaka 2 mwenye ufahamu mkubwa anayedai kusoma ‘UDOM’ (Video)


 Mtoto mwenye umri wa miaka miwili, Ithan Mahafudh, amethibitisha kuwa na kipaji kikubwa kinachowashangaza wengi, baada ya kuonekana akiwa na ufahamu mkubwa, pamoja na kukariri vitu ambavyo kwa umri wake, siyo jambo la kawaida. Mtoto huyo, licha ya kukariri, lakini pia anao uwezo wa kuwataja majina viongozi mbalimbali duniani, wakiwemo mawaziri wa serikali ya Rais Dk John Pombe Magufuli. Ijumaa lilitinga nyumbani kwa wazazi wa Ithan huko Uwanja wa Ndege, Bukoba Mjini, lilifanya mahojiano na wazazi hao ambapo walifungukia kipaji cha mtoto wao kama ifuatavyo;
                                                   Ithan Mahafudh akiwa na wazazi wake.
BABA MAHAFUDH LUSHAKA
“Naitwa Mahafudh Lushaka, ni mtumishi wa Serikali katika mamlaka ya viwanja vya ndege, kiukweli mimi kwa mara ya kwanza niliona ni mambo ya kawaida kabisa, sikujua kama ni kipaji na sikudhani kama angekuwa maarufu hivi, kwani nakumbuka tukiwa nyumbani alikuwa na kawaida ya kupenda kuangalia runinga, vipindi vya taarifa za habari na huwa anafuatilia kwa umakini vitu vya maana.

“Anapenda kubadili vipindi, lakini mara kwa mara anaangalia vipindi vya watu wazima vinavyohusu jamii na serikali kwa ujumla, anapenda kudadisi na kujua mambo na kukariri, kama akiona kitu hakielewi anauliza.
“Siku moja nilimsikia akikariri, tulipokwenda kulala nikaanza kumuuliza maswali nikitaka kumpima ufahamu wake, akawa anarudia majina yote ya marais hata wa nje ya nchi, nikashangaa.

 “Hata hivyo, sikutilia maanani zaidi, ndipo nikiwa kazini nikawa naona watu wanamrekodi na kutupia mtandaoni, lakini mimi na mama yake Warda Nchambizi hatukuwahi kufanya hivyo.
“Watu walituambia kuwa mtoto wetu ana kipaji kikubwa kwani umri wake ni mdogo kuweza kukariri majina yote hayo, ndipo nilipofunguka hasa baada ya kuwa gumzo kubwa mitandaoni.

WATU WAJAA NYUMBANI KWAO
“Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo watu wanavyozidi kufika na kujazana nyumbani kwao, wengi wakitaka kupiga picha na mtoto na wengine wakimrekodi.
“Waandishi wa habari walipokuja kumuona na kutuhoji ndipo niliamini kweli mwanangu anao ufahamu mkubwa.”

ANA-DRIVE, ‘ETI’ ANASOMA UDOM!
Maajabu mengine ya mtoto Ithan ni kuwa anafahamu kuendesha gari na pia anajua kutumia kompyuta na simu za kisasa yaani smartphones, kwani anao uwezo wa kuingia katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Katika tukio lingine, mtoto huyo akiulizwa anasoma wapi, anajibu kuwa anasoma Udom (Chuo Kikuu cha Dodoma) wakati hajaanza hata chekechea!

MPANGO WA SHULE VIPI
Ithan hasomi shule yoyote kutokana na umri wake, wazazi wake walipanga kumpeleka shule atakapotimiza miaka mitatu.

                                                               Mtoto Ithan Mahafudh.
Nyumbani kwa akina Ithan Mahafudh.

KUHUSU MALEZI YAKE?
Mama yake ni mfanyabiashara soko la mjini Bukoba, amekuwa akimlea mwenyewe na amekuwa akimuepusha kukaa na kundi la watoto wenzake kwa hofu ya kupata tabia mbaya kwani uelewa wake mkubwa wa kukariri mambo unaweza kusababisha akakariri maneno mabaya yakiwemo matusi.
“Tumekuwa tukimuepusha kukaa na watoto zaidi kwa sababu kama alivyo na ufahamu wa kukariri ni rahisi kukariri na matusi kitu ambacho nakiepusha sana,” alisema Warda mama mzazi wa Ithan.

“Watu wamenishauri mtoto awekewe ulinzi, mimi naona ni mapema mno kwani Mungu ndiye anamlinda ingawa kuna tukio moja lilitukuta baada ya kutolewa kwenye runinga.
“Tulienda eneo moja linaitwa Rwamishenye, huko aliposhuka tu kwenye gari watu walimvamia na kuanza kumuuliza maswali, ilikuwa shida sana kurudi garini kwa sababu walimzuia ikabidi niwaambie nitawaita askari ndiyo wakamwachia, tunapata usumbufu mkubwa kwa kweli,” anasema baba wa mtoto huyo.

Makala: Abdullatif Yunus, Kagera na Hamida Hassan, Dar

No comments

Powered by Blogger.