Mavugo, Ajibu waandaliwa kuwapoteza Ngoma, Tambwe

MASTRAIKA wa Simba, Ibrahim Ajib na Laudit Mavugo, wanaandaliwa kuja
kuwa wafungaji wazuri kwenye Ligi Kuu Bara huku wakibebeshwa zigo la
kuvunja utawala wa mastraika wa Yanga, Amissi Tambwe na Donald Ngoma.
Kikosi cha Simba msimu uliopita kilikuwa kikimtegemea zaidi Mganda,
Hamisi Kiiza katika safu yao ya ushambuliaji. Nyota huyo  alimaliza
msimu akiwa na mabao 19, nyuma ya Tambwe aliyeibuka mfungaji bora kwa
kufunga mabao 21.
Mpaka sasa tayari Kocha wa Simba, Joseph Omog, ameshatengeneza
kombinesheni ya hatari ya safu yake ya ushambuliaji ambapo Ajib na
Mavugo ndio watakuwa wakicheza pamoja kwa muda mwingi huku Muivory
Coast, Fredric Blagnon na Danny Lyanga wakisubiri.
Katika kuitengeneza kombinesheni hiyo, Omog amekuwa akiwafundisha mabeki
wake wa pembeni pamoja na mawinga kupiga krosi nyingi kuwafikia
washambuliaji hao. Kwenye mazoezi yao ya kila siku, wamekuwa wakifanya
hivyo na zoezi hilo kuonekana kueleweka.
Omog ameliambia Championi Jumatatu kuwa, kila siku anaangalia namna gani
timu yake itakuwa inapata ushindi kwa urahisi na kugundua kwamba mipira
ya krosi itawabeba zaidi.
“Kuna njia nyingi za kusaka ushindi, mara kwa mara nimekuwa
nikiwafundisha hivi na kuonekana kuelewa zaidi, hivyo naamini hii ndiyo
itakuwa rahisi kwetu kupata mafanikio msimu ukianza. Nataka kutengeneza
safu bora zaidi ya ushambuliaji kwenye ligi,” alisema Omog.

No comments

Powered by Blogger.