Majimaji Selebuka watu kuogelea mamilioni

                                          
Na mwandishi Wetu
JUMAPILI ya wikiendi hii, tamasha la kila mwaka la Majimaji Selebuka litaanza kutimua vumbi, ukiwa ni msimu wake wa tatu tangu lizinduliwe na burudani yote itakuwa kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea-Ruvuma.
Habari njema ni kwamba tofauti na misimu ya awali, safari hii ni mwendo wa washindi kujichotea mamilioni ya fedha wakiongozwa na riadha mbio za 42km ambazo kinara atakunja kitita cha milioni moja.
Tamasha hilo linaloratibiwa na Mwandi Tanzania kwa ushirikiano na Asasi ya Songea & Mississippi (Somi), lengo kuu ni kuibua vipaji mbalimbali vya michezo, kumuinua mwananchi wa kawaida kiuchumi kupitia elimu na maonyesho ya ujasiriamali pamoja na udumishaji wa mila na desturi asilia za mkoa wa Ruvuma.
Kwa mujibu wa Mratibu Mkuu, Reinafrida Rwezaula pia kutakuwa na mbio za 2.5km (kwa wototo), 5km, 10km na za 21km na mbio za walemavu.
“Tofauti na misimu iliyopita, safari hii tumeboresha tuzo ambako zipo mpaka za milioni moja kwa upoande wa mbio ndefu. Tumeandaa fursa za washiriki kwenda kupata kozi za kimataifa kwa mchezo wa mbio za baiskeli na mengine mengi,” alisema Reinafrida.
Ameiomba serikali kutupia jicho kwa ajili ya kupata vipaji vya michezo mbalimbali mfano kama riadha ambako timu ya taifa ikijiandaa na mashindano ya Olimpiki ya 2020.
Mbio za baiskeli ni za 100km kutoka Mbinga mpaka Songea mjini ambako washindi watatu watapata dili la kozi ya kimataifa ya mchezo huyo na plani ya kwanza ni kuwapeleka ‘Sauzi’ kama ilivyokuwa kwa washindi wa mwaka jana ama waende Rwanda.
Michezo mingine ni mashindano ya ngoma za asili, vipaji vya uchoraji kwa watoto kupitia Jukwaa la Mtu Kwao na shughuli za kijamii kama utalii wa ndani, midahalo kwa shule za sekondari na maonyesho ya ujasiriamali kwa bidhaa zitokanazo na rasilimali mkoani Ruvuma. Shule tatu zitajishindia Kwa washindi wa mdahalo, shule zitakabidhiwa IPad zenye notisi kidato cha kwanza mpaka cha sita kwa masomo yote.
Tamasha hilo litadumu wiki moja mpaka Julai 30, mwaka huu. Fomu za ushiriki bado zinapatika kupitia tovuti za www.majimajiselebuka.com au www.majimajiselebuka.wordpress.com

No comments

Powered by Blogger.