Meya wa jiji la DSM kusaidia deni la Makaburi ya Tambaza

 Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita, akihutubia Umma wa kislamu  uliofika katika dua maalum ya  kumuombea  Shekhe Yahya Hussein  pamoja na kukaribisha mwezi mtukufu Ramdahani unaotarajia kuanza mwishoni mwa wiki hii. Dua hiyo ilifanyika   katika Makaburi ya Tambaza Jijini Dar es salaam jana
 Baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu waliohudhuria   dua maalumu ya kuwaombea marehemu na vipenzi vya Mtume Muhamad (s.a.w) iliyofanyika jana katika makaburi ya Tambaza, Upanga Mashariki jiji Dar es Salaam
 Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita, akiwa kwenye dua ya pamoja na baadhi ya mashehe waliohudhuria dua maalumu ya kumuombea Sheikh Yahya Hussein sambamba na kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Dua hiyo ilifanyika jana katika makaburi ya Tambaza yaliyopo Upanga Mashariki jijini hapa.
 Mstahiki Meya Isaya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita mjukuu wa marehemu Shekhe Yahya Hussein, Yahya Hussein wakati akisoma Quruan Tukufu  katika Makaburi ya Tambaza Jijini Dar es salaam jana
 Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita, akipokea risala maalumu iliyoandaliwa na Taasisi ya Shekhe Yahya Hussein katika dua maalumu  ya kumuombea Shekhe Yahya Hussein pamoja na kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani  katika  makaburi ya Tambaza yaliyopo Upanga Mashariki Jijini Dar es salaam jana
  Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita, akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya mashekhe wa taasisi hiyo.

NA CHRISTINA MWAGALA, OFISI YA MEYA WA JIJI
MSTAHIKI Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita ameahidi kusaidia kupunguza deni la sh. Milioni 16 linalodaiwa na mkandarasi wa kampuni ya Ushirombo kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa makaburi ya Tambaza.
Meya Isaya alisema kuwa kwa nafasi yake atajitahidi ili kuhakikisha kwamba anasaidia kupunguza deni hilo kama sio kumaliza kabisa kutokana na umuhimu wa watu ambao wamepumzishwa katika eneo hilo.
Meya Mwita aliyasema hayo jijini hapa jana wakati wa dua maalumu ya kumuombea Sheikh Yahya Hussein sambamba na kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema kwamba hafanyi jambo hilo kwa ajili ya mambo ya kisiasa ama kuwafurahisha waislam, bali ni kutokana na kutambua umuhimu wa watu waliolala katika eneo hilo, hasa ukizingatia kila mwanadamu lazima apitie hatua hiyo.
“ Nimesikia kwenye risala yenu kuwa mnadeni ambalo ni kubwa, lakini mimi sitasema nitachangia kiasi gani, ila nitapunguza kwa nafasi yangu kiasi ambacho mnadaiwa” alisema Meya Mwita.
“ Watu ambao leo hii tunawakumbuka wamelala hapa, walikuwa na mchango mkubwa , kila mmoja anatambua hilo, waliweza kuitangaza  nchi yetu kwenye mambo ya dini , lakini pia kwenye mambo mengi ya kimaendeleo , hivyo tunatakiwa kutambua na kuwakumbuka” aliongeza.
Aidha katika hatua nyingine , Meya Mwita aliwasihi waumini wa dini ya kiisilamu , katika kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuwaeleza kwamba ni muhimu kuendeleza mambo mema ambayo huyafanya wakati wa mfungo huo.
Alifafanua kwamba , imekuwa ni kawaida kwa muislam kutumia kipindi cha mfungo wa ramadhani kuficha maovu na kutenda mema ,lakini baada ya kumaliza kipindi hicho huendelea na matendo yasiyompembeza muumba wao.
Alisema ifike wakati kwa kila muumini ,kutambua umuhimu wa kutenda na kuendeleza mema ambayo aliyafanya wakati wa mfungo kwani kufanya hivyo kutamuweka kwenye nafasi nzuri ya kiimani.
“ Kuna jambo ambalo ndugu zangu waislam huwa mnafanya, wakati wa mwezi kama huu ambao tunaelekea, kila muislam utamuona akihusisha kwenye mambo mema tu, wale ambao walikuwa hawaswali wataenda msikitini, wale ambao walikuwa wakitenda mambo machafu ya kumchukiza muumba wao wataacha”
Lakini baada ya kipindi hicho cha siku 30 kumalizika kila mmoja atarudi kwenye tabia yake, sasa hili jambo ni mtihani kwa kweli, niwasihi tu, najua naongea maneno machungu , na nina wagusa wengi, tujenge utamaduni wa kuyaendeleza haya badala ya kuacha” alisisitiza Meya Mwita.
Hata hivyo  Mashehe waliohudhuria dua hiyo, walimpongeza Meya Mwita kwakuwa na moyo wa kujitoa kwenye shuguli za kijamii na hivyo kumuomba kuendelea na misingi hiyo ili aweze kuwatumikia vizuri wananchi wa jiji analoliongoza.

No comments

Powered by Blogger.