Huyu Hapa Kikongwe Mwenye Miaka 145 na Bado Anavuta Sigara

 Mzee Mbah Gotho raia wa Indonesia anaamini yeye ndiye binadamu mzee zaidi kuwahi kuishi duniani kwani ameishi miaka mingi zaidi kuliko wake zake wanne, ndugu zake 10 na wanawe wote ambao wamekwisha fariki dunia.
 Mjukuu wa Mzee Gotho aitwaye Suryanto ameeleza kuwa kwa mujibu wa nyaraka za serikali, babu yake huyo alizaliwa katika Kisiwa cha Java ya Kati mnamo Desemba 31 mwaka 1870 na kuongeza kuwa mpaka sasa bado anaendelea kuvuta sigara ingawa umri wake ni mkubwa (miaka 145).
  Mbali na mjukuu wake huyo, ofisa mmoja wa serikali naye alithibitisha umri wa mzee Gotho kwa kusema, “Tunaamini stakabadhi hizi ni halali, kwa mujibu wa nyaraka rasmi za serikali. Tunaamini tarehe yake ya kuzaliwa ni sahihi,” anasema afisa wa serikali Wahyu Wiyanto.
Akihojiwa na BBC, mzee Gotho alisema,
 “Huwa najaribu kuwa mvumilivu na kuamini kuwa kuna watu watakaonitunza, nimeishi muda mrefu kwa sababu nina watu wanaonipenda na kunitunza.” Alisema mzee Gotho.
Serikali ya Indonesia ilianza kunakili rasmi kuzaliwa kwa watu miaka ya 1900, hivyo ni vigumu kuthibitisha tarehe kamili ya watu waliozaliwa kabla ya hapo.
Katika jamii ambayo Mbah Gotho anatoka, wenyewe humchukulia kama shujaa wao huku akiwa ametunza kumbukumbu ya matukio makubwa yaliyowahi kutokea enzi za ukoloni na maisha yake kwa ujumla.
 “Siku ya Uhuru alikuwa akialikwa kusimulia yaliyotokea wakati wa vita. Anaweza kusimulia kuhusu vita dhidi ya wakoloni kutoka Japan na Uholanzi,” anasema Wahyu Wiyanto.
Mjukuu wake anasema mzee huyo huwa hana masharti mengi na huwa halazimishi kupewa chakula maalum kama walivyo vikongwe wengine.
“Kitu pekee alitutaka tufanye ni kununua jiwe la kaburi lake,” anasema.
Mzee huyo anasema kwa sasa anaishiwa na nguvu na hatarajiwi endapo ataishi miaka mingi zaidi ijayo.
“Sina nguvu kama zamani. Hata kutembea ni shida. Nilikuwa mkulima na nilivua samaki mtoni. Sitaki kuendelea kuishi sana, ndio maana nimeandaa kaburi. “Ili nikifariki, kila kitu kiwe tayari,” anasema Gotho.
“Kwa sasa nataka tu kufariki, lakini wakati wangu haujafika bado.”
Mtu ambaye aliishi miaka mingi zaidi duniani kulingana na Guinness ni Jeanne Calment kutoka ufaransa ambaye aliishi miaka 122 na siku 164 . Aliaga dunia mwezi Agosti mwaka 1997.

No comments

Powered by Blogger.